Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amempongeza Askofu
mkuu mstaafu Desmond Tutu kwa kupewa tuzo la heshima la Templeton, tukio ambalo linatambua
mchango wa Askofu mkuu mstaafu Tutu katika kusimama kidete kulinda na kutetea misingi
ya matumaini, upatanisho sanjari na kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi vilivyokuwa
vinafanyika chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi, Afrika ya Kusini.
Dr. Tveit
amempongeza Askofu mkuu mstaafuTutu kwa kazi kubwa aliyoifanya wakati wa utume wake
Kiongozi mkuu wa Kanisa Afrika ya Kusini, mwanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni
na Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Afrika ya Kusini. Askofu mkuu Tutu alipokea tuzo
hii hivi karibuni akiwa mjini London. Askofu mkuu mstaafu Tutu alikuwa ni "mwiba"
na moto wa kuotea mbali wakati wautawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini uliokuwa
umepamba moto kati ya mwaka 1970 hadi mwaka 1980.
Baada ya kuanguka kwa utawala
wa ubaguzi wa rangi, Askofu mkuu mstaafu Desmond Tutu alipewa dhamana ya kuwa ni Mwenyekiti
wa Tume ha Ukweli na Upatanisho nchini Afrika ya Kusini iliyoundwa kwenye miaka ya
1990. Tume hii ilisaidia kushinda kinzani, migawanyiko na utengano uliokuwepo miongoni
mwa wananchi wa Afrika ya Kusini.
Askofu mkuu mstaafu Desmond Tutu, alisaidia
kuendeleza mchakato wa mabadiliko katika demokrasia. Ni kiongozi aliyesimama kulinda
na kutetea haki msingi za binadamu; akaongoza mchakato wa majadiliano katika ukweli
na uwazi; akapinga ubaguzi wa rangi, fujio na vurugu kwa kukazia umuhimu wa kujenga
na kuimarisha majadiliano na umoja, akawa ni mfano wa kuigwa katika kudumisha haki
na amani.
Dr. Tveit anasema kwamba, Askofu mkuu Tutu alitetea ile sura na mfano
wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, akataka kila mtu aheshimiwe na kuthaminiwa si
kutokana na rangi yake, bali kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Tuzo
ya Templeton, ilianzishwa kunako mwaka 1972 na Hayati John Templeton aliyependa tuzo
hii itolewe kwa watu watakaochangia kwa kwa njia mbali mbali katika kukuza na kudumisha
mwelekeo wa maisha ya kiroho.