2013-06-20 08:55:58

Waraka kuhusu Sala ya Ekaristi kwa Mtakatifu Yosefu!


Baraza la Kipapa la Nidhamu na Sakramenti za Kanisa katika kikao chake cha tarehe Mosi, Mei, 2013 limetoa Tamko ambalo linaingiza jina la Mtakatifu Yosefu mara baada ya kutaja jina la Bikira Maria Mama wa Mungu katika Sala ya Ekaristi ya: II, III na IV mintarafu Toleo la tatu la Misale ya Kirumi ambalo kwa sasa limetafsiriwa katika lugha mbali mbali.

Mama Kanisa anatambua mchango na dhamana kubwa aliyotekeleza kwa uaminifu Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wa Familia Takatifu ya Nazareti. Ni mtu aliyesimama imara katika Fumbo la Mpango wa Mungu wa ukomboi tangu mwanzo kabisa, akawa ni mfano na kielelezo cha upendo na unyenyekevu; fadhila ambazo Imani ya Kikristo inazipatia kipaumbele cha juu na ambazo zinaonesha katika hali halisi na ya kawaida mambo ambayo yanaweza kuwasaidia waamini kuwa ni wafuasi makini wa Kristo.

Kwa njia ya fadhila hizi, Yosefu, mtu wa haki, aliyemtunza kwa upendo mkuu Bikira Maria Mama wa Mungu, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumlea Yesu; kwa njia hii akawekwa kuwa ni mtunzaji wa amana ya Mwenyezi Mungu. Yosefu amekuwa ni mfano na kielelezo cha ibada kutoka kwa Watu wa Mungu katika historia ya Kanisa na msaada mkubwa wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Waamini wa Kanisa Katoliki wameendelea kuonesha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu na kwamba, wameendelea kuadhimisha kumbu kumbu yake kama Mume wa Bikira Maria Mama wa Mungu na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Kutokana na sababu hizi, Papa Yohane wa Ishirini na tatu katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alitamka wazi kwamba, Jina la Mtakatifu Yosefu liongezwe kwenye Kanuni ya Misa ya Kirumi.

Kutokana na maombi yaliyoletwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alikubali jina hili liingizwe na sasa limeridhiwa na Papa Francisko. Uamuzi huu umefanywa wakati ambapo Baba Mtakatifu ansona umoja wa Watakatifu waliofanya hija ya maisha yao hapa duniani na sasa wanawaongoza waamini kwa Kristo ili waweze kujiunga naye.

Kuanzia sasa Baraza la Kipapa la Sakramenti za Kanisa na Nidhamu kwa mamlaka lililokabidhiwa na Baba Mtakatifu Francisko linatamka wazi kwamba, Jina la Mtakatifu Yosefu liongezwe katika Sala ya Ekaristi ya II, III na IV kama inavyojionesha kutoka katika Kitabu cha Misale ya Kirumi baada ya kutaja Jina la Bikira Maria Mama wa Mungu kama ifuatavyo katika Sala ya Ekaristi ya Pili: "Maria Bikira Mwenyeheri Mama wa Mungu, Mtakatifu Yosefu, muwe wake, mitume wenye heri..."

Katika Sala ya Ekaristi ya III itasomeka kama ifuatavyo: Bikira Maria Mwenyeheri, Mama wa Mungu, Mtakatifu Yosefu mume wake na mitume..."

Katika Sala ya Ekaristi ya IV itasomeka: "Bikira Maria Mwenyeheri, Mama wa Mungu na mitume...". Sala hii katika Lugha ya Kilatini inatamkwa wazi kuwa ni maalum. Baraza la Kipapa linatarajia kutoa tafsiri kwa lugha zinazotumiwa zaidi na nchi za Magharibi; tafsiri nyingine zitafanywa na Mabaraza ya Maaskofu katoliki mintarafu sheria, na kuthibitishwa na Vatican kupitia Baraza hili.

Tamko hili limetolewa na Kardinali Antonio Canizares Llovera, Mwenyekiti pamoja na Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu.







All the contents on this site are copyrighted ©.