2013-06-20 07:59:39

Shangwera ya Fedha: Askofu Mkude Miaka 25 ya Uaskofu


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, toba na msamaha anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Itakumbukwa kwamba, Askofu Mkude alizaliwa tarehe 30 Novemba 1945, Pinde, Jimbo Katoliki la Morogoro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, kunako tarehe 16 Julai 1972 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. RealAudioMP3

Tarehe 18 Januari 1988 akateuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga. Tarehe 26 Aprili 1988 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga. Kunako tarehe 5 Aprili 1993, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro.

Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, Askofu mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye asili ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa na kwamba, ndiye anayemwezesha mja wake ili aweze kuwa ni chombo cha kutekelezea malengo yake. Mwenyezi Mungu anatumia njia mbali mbali kuita baadhi ya watu kwa ajili ya wito wa Kipadre. Vijana hawa husaidiwa na familia, walimu na walezi wao kukuza miito yao.

Askofu Mkude anasema, baada ya mwalimu wao kuwafafanulia shule mbali mbali, alionekana kuvutwa zaidi na Seminari Ndogo ya Bagamoyo, kwani hapa aliambiwa kwamba, kilikuwa ni kitalu cha kutayarisha Mapadre na kwamba, Waseminari waliotoka Bagamoyo walionekana kuwa ni vijana wenye heshima na adabu njema mbele ya Jamii pale Kijijini kwao, jambo hili likaleta mguso zaidi kwani hata yeye alitamani kuwa ni kati ya vijana wenye sifa na adabu njema Kijijini mwake.

Baada ya Upadrisho alimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie kutekeleza mambo makuu matatu: kutokataa kuhama, kutoomba kwenda kusoma na mwisho kutoomba kuhama. Yote haya yanajikita katika msingi wa utii na unyenyekevu.

Askofu Mkude anasema kwamba, hakuna formu ya maombi ya Uaskofu, bali Kanisa linamwomba Padre kusaidia jitgihada za Mama Kanisa katika kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu. Alipoombwa kwenda Tanga kama Askofu, hakusita na akajisemea moyoni mwake, "Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu". Kama Askofu kwa Jimbo Katoliki la Tanga na Morogoro ameonja upendo, utii na unyenyekevu wa Familia ya Mungu, changamoto inayomsukuma kuendelea kujinyenyekeza zaidi kwa ajili ya kuwahudumia.

Anasema, katika maisha yake kama Padre na Askofu ameguswa kwa namna ya pekee na mafanikio yaliyooneshwa na Mapadre na Maaskofu wenzake katika medani mbali mbali za maisha; wakafanikiwa kwa kiwango na ubora! Anasema siri ya mafanikio yao ni kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba, wamekuwa pia ni watu wa sala na upendo mkuu kwa watu waliokabidhiwa kwao, wakatekeleza dhamana na utume wao kwa moyo mkuu na mnyofu bila kubagua! Kwa hakika hawa ni watu ambao wanamtegemea Mungu katika maisha na utume wao!

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 25 ya Uaskofu anamshukuru Mungu na kumwomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume wake. Anawawaomba wote walioguswa kwa namna ya pekee na huduma na maisha yake kama Padre na Askofu wajiunge pamoja naye ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Anawaomba wale ambao wameguswa kwa namna hasi na maisha yake kama Padre na Askofu, wamsamehe na kuungana naye kumwomba Mwenyezi Mungu toba na wongofu wa ndani.

Askofu Mkude anasema, Kristo ndiye tumaini lake na kwamba anamtegemea Yeye ambaye ni Kristo na Bwana! Usikose kujiunga na ukurasa huu, tutakapokuletea salam na matashi mema kutoka kwa Maaskofu Katoliki Tanzania, wakati huu, Askofu Telesphor Mkude anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 25 ya Uaskofu







All the contents on this site are copyrighted ©.