Saidieni Familia za Wakimbizi, ili waonje upendo na ukarimu wenu!
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni inaadhimisha Siku ya Wakimbizi
Duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wakimbizi na Familia zao wanapaswa kusaidiwa
kwa hali na mali na kwamba, kila hatua ya maisha ya binadamu inapaswa kulindwa, kutunzwa
na kuheshimiwa.
Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo wakati wa Katekesi
yake, Jumatano, tarehe 19 Juni 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican, uliokuwa umefurika kwa umati mkubwa wa waamini, mahujaji na watu wenye
mapenzi mema.
Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kuna wakati ambapo wakimbizi
wanalazimika kuzikimbia nchi zao kwa kuacha kila kitu ili kuokoa maisha yao. Madhulumu,
ubaguzi, maafa asilia na vita ni kati ya mambo ambayo yanapelekea watu wengi kuzikimbia
nchi zao.
Hata katika mazingira kama haya, bado familia zinaweza kujikuta
zikiwa zimetengana sanjari na kukabiliwa na hali ngumu zaidi ya maisha, changamoto
kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwaonjesha mshikamano wa upendo kwa kuwahudumia,
kwani wao ni kielelezo cha uso wa Kristo Mteswa!
Baba Mtakatifu akiwa bado
na kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Injili ya Uhai kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda
na kutetea Injili ya Uhai katika hatua zake zote kadiri ya mpango wa Mungu. Waamini
wawe ni mashahidi wanaoipokea Injili ya Uhai, Waishuhudie na kuitangaza hadi miisho
ya dunia, kwani kila Mkristo anadhamana ya kuikumbatia Injili ya Uhai.
Shirika
la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu
millioni 45 waliolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao, sehemu mbali mbali za dunia.