2013-06-20 13:58:32

Papa Francisko kukutana na Mabalozi wanaowakilisha Vatican sehemu mbali mbali za dunia!


Mabalozi na wawakilishi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakutanika mjini Vatican siku ya Ijumaa, tarehe 21 hadi tarehe 22 Juni 2013 kuadhimisha Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Hii itakuwa ni nafasi kwa Mabalozi wa Vatican wanaotekeleza wajibu na utume wao sehemu mbali mbali za dunia kubadilishana mawazo, uozefu na mang'amuzi katika maisha na wito wao kama wawakilishi wa Vatican.

Kwa mara ya kwanza tukio kama hili lilifanyika kunako mwaka 2000, wakati wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Ukristo, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Ratiba inaonesha kwamba, Ijumaa asubuhi watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Jioni, watapata fursa ya kusali Masifu ya Jioni pamoja na Kuabudu Ekaristi Takatifu. Masifu yataongozwa na Kardinali James Michael Harvey na Kardinali Giafranco Ravasi atatoa tafakari ya Neno la Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma.

Mabalozi hawa watetembelea mapamgo ya Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma. Jioni watakula chakula cha pamoja na Baba Mtakatifu Francisko.

Ratiba ya Jumamosi, asubuhi, tarehe 22 Juni 2013, inaonesha kwamba, Mabalozi wa Vatican, wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, itakayoongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Baadaye, watakutana na kuzungumza na viongozi wakuu waandamizi kutoka katika Sekretarieti ya Vatican. Mchana watapata chakula pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Makazi yake ya muda Domus Sanctae Marthae. Jumamosi jioni, watashiriki tamasha la muziki lililoandaliwa kwa niaba yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.