Kuomba kwa Baba Yetu wa mbinguni ni lazima mioyo yetu iwe na amani na ndugu zetu.
Papa Francisko, alieleza mapema asubuhi wakati wa Ibada ya Misa, aliyoiongoza
katika Kikanisa kidogo cha Mtakatifu Marta mjini Vatican. Papa alisisitiza kuwa,
tunaamini katika Mungu ambaye ni Baba, na ambaye yupo karibu nasi , si kama ni Mungu
wa kufikirika au miungu hewa ya kidunia.
Katika Misa hiyo, Papa aliiongoza
akisaidiana na Kardinali Zenon Grocholewski na miongoni mwa wengine walioshiriki
ni kundi la washirika wa Usharika kwa Elimu Katoliki na kundi la wafanyakazi wa Makumbusho
ya Vatican.
Papa Fransisko alieleza katika homilia yake kwamba, Maombi si
uchawi, lakini ni kujiweka kwa uaminifu katika mkono wa Mungu. Papa, ililenga zaidi
katika mafundisho ya Yesu kwa wanafunzi wake, kama ilivyoelezwa katika somo la Injili
ya Siku hii. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake jinsi ya kusali na si kutoa maneno
mengi tu na kelele nyingi batili.
Papa alitoa onyo kwa wale wanaofikiria kwamba
maombi na sala ni sawa na uchawi akisema, Maombi si uchawi bali ni kuwa tayari kukumbatiwa
na Mungu . Hakuna uchawi hata katika sala za uponyaji bali ni majitoleo ya kuzungumza
na Mungu na kumwambia yanayo tusibu tukiwa tumejawa na imani kwake. Hivyo fikara
za kuona kama maombi ni uchawi hizo ni fikira za kipagani.
Papa alieleza na
kurejea jinsi Yesu alivyo wafundisha wanafunzi wake kusali akisema, sala haipaswi
kuwa ya maneno mengi na kupayukapayuka, kwa kuwa Yeye anajua kila kitu. Aliongeza
neno la kwanza katika sala ni Baba. Baba ni ufunguo wa sala . Ni lazima kumwomba Baba
ambaye yote yanatoka kwake na mwenye kujua maisha yetu yote. Na hivyo hatuwezi kumwomba
kwa midomo yetu tu lakini maombi yanapaswa kutoka ndani ya moyo safi usiokuwa na kinyongo
kwa miwngine kwa kuwa Yeye nI Mungu wa Upendo.