2013-06-19 10:15:41

Wananchi vijijini wanapaswa kuwezeshwa ili kujikwamua kutokana na hali mbaya ya maisha!


Mfuko wa Maendeleo ya watu, "Populorum Progressio ulioanzishwa kunako mwaka 1992 na kuwekwa chini ya Baraza la Kipapa linaloratibu misaa ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, umeanza mkutano wake mkuu wa mwaka hapo tarehe 18 Juni na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 21 Juni 2013 mjini Arequipa, Peru. Mkutano huu unafanyika chini ya usimamizi wa Kardinali Robert Sarah, Rais wa Cor Unum.

Mkutano huu unafanyika kwa mara ya kwanza tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, ambaye tangu mwanzo ameendelea kulihamasisha Kanisa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anasema, huduma ya upendo haina budi kupewa kipaumbele cha kwanza na Kanisa katika mikakati na shughuli zake za kichungaji. Walengwa wakuu wa Mfuko wa Maendeleo ya watu ni wananchi wanaoishi vijijini huko Amerika ya Kusini.

Amerika ya Kusini inaendelea kucharuka kwa maendeleo makubwa, lakini kuna hatari kwamba, wananchi wanaoishi vijijini wataweza kusahaulika kutokana na mchakato huu kutokana na mikakati tenge ya maendeleo. Viongozi wakuu wa Mfuko huu, hapo mwakani, wamepania kwamba, mkutano wao wa mwaka ufanyike mjini Vatican ili waweze kupata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuwashirikisha vipaumbele, dira na mwongozo wa Mfuko huu kwa siku za usoni.

Kuna mradi 222 inayojadiliwa kwa sasa kutoka katika nchi 18 za Amerika ya Kusini. Hii ni miradi shirikishi inayowahusisha wananchi wa kawaida tangu mwanzo hadi utekelezaji wake. Lengo ni kusaidia juhudi za wakulima wadogo wadogo kuinua kiwango cha tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo; kazi za mikono, biashara ndogo ndogo; miundo mbinu ya kijamii, elimu, afya na ujenzi wa miundo mbinu: majengo. Wafadhili wakuu wa Mfuko huu ni Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.







All the contents on this site are copyrighted ©.