SADC yaomba kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi nchini Zimbabwe!
Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, wameiomba Serikali ya Umoja
wa Kitaifa nchini Zimbabwe kuahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe
31 Julai 2013 ili kupunguza kinzani ambazo zimejitokeza kati ya Rais Robert Mugabe
na Waziri mkuu Bwana Morgan Tsvangirai.
Chama cha Upinzani kinamshutumu Rais
Mugabe kwa kutia sahihi waraka wa serikali kuhusu mabadiliko ya uchaguzi, kitendo
kinachovunja makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa kuhusu ugawanaji wa madaraka katika
Serikali ya Umoja wa Kitaifa. SADC inapendekeza kwamba, uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe
ufanyike tarehe 25 Agosti 2013.
Lakini pendekezo hili linapaswa kupelekwa
kwenye Mahakama kuu ya Zimbabwe ili iweze kutoa uamuzi wa kisheria. Ni matumaini ya
SADC kwamba, uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe hautakuwa tena chanzo cha migogoro na kinzani
nchini Zimbabwe.
Wachunguzi wa mambo wanasema, pengine shutuma hizi hazina
msingi, ikiwa kama Serikali ya Kitaifa ilikuwa na muda wa miaka minne na nusu kuweza
kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi na haikuweza kufanikisha yale yaliyokuwa
yanakusudiwa, itawezekanaje kuharakisha masuala haya katika kipindi cha mwezi mmoja
tu?