ONU inasikitishwa na idadi kubwa ya watoto nchini Mali kuwekwa kizuizini!
Umoja wa Mataifa umeonesha wasi wasi wake kutokana na ongezeko la watoto nchini Mali
kuwekwa kizuizini kwa kizingizio kwamba wanashirikiana na Kikundi cha Waasi kinachoendesha
shughuli zake Kaskazini mwa Mali. Akizungumza kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa Bi Leila Zerrougui, Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika maeneo yenye
kinzani na vita, anasema kwamba, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko
la watoto wanaoteseka kutokana na kuwekwa kizuizini.
Umoja wa Mataifa unataka
haki msingi za watoto hao ziheshimiwe kadiri ya sheria na kanuni za kimataifa, jambo
ambalo linapaswa kutekelezwa na Serikali ya Mali. Kuna dalili nyingi kwamba, nchini
Mali haki za watoto zinaendelea kuvunjwa kwa kuwafundisha watoto ili kujiunga na vikosi
vya kijeshi ili hatimaye, kupelekwa mstari wa mbele kwenye mapambano.