2013-06-19 10:31:59

Monsinyo Battista Ricca ateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Tume ya Makardinali inayosimamia na kuratibu Benki ya Vatican


Tume ya Makardinali inayosimamia na kuratibu shughuli za Benki ya Vatican IOR imemteua Monsinyo Battista Mario Salvatore Ricca kuwa katibu mkuu wa Tume ya Makardinali inayosimamia Benki ya Vatican na uteuzi huu kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, atahudhuria mikutano ya Taasisi hii ya fedha ya Vatican kadiri ya sheria na kanuni za IOR. Hayo yamefafanuliwa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican hivi karibuni.

Monsinyo Battista Ricca ni kati ya viongozi waandamizi wa huduma ya kidiplomasia mjini Vatican pia ni mkurugenzi mkuu wa Nyumba za Mapadre zinazomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Monsinyo Ricca anachukua nafasi ya Askofu mkuu Pierro Pioppo aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Cameroon na Equatorial Guinea. Yeye alikuwa ni Katibu wa Tume ya Makardinali kwa ajili ya Benki ya Vatican kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2010.

Kwa uteuzi wa Bwana Ernst Von Freyberg kuwa Rais wa Benki ya Vatican na sasa uteuzi wa Monsinyo Battista ricca, Tume ya Makardinali imeziba mwanya wa uongozi wa Benki ya Vatican; nafasi ambayo ilikuwa wazi kwa muda kadhaa.







All the contents on this site are copyrighted ©.