2013-06-18 09:04:31

Vyombo vya habari vina dhamana ya kulinda na kukoleza misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu!


Vyombo vya upashanaji habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Wakristo Mashariki ya kati havina budi kujielekeza zaidi katika huduma inayopania kuendeleza mchakato wa haki na amani na kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na wote wanaoteseka kutokana na kinzani za kisiasa, kijamii na kidini huko Mashariki ya Kati.

Mama Kanisa anaendelea kuwahamasisha Wakristo na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanalisaidia Kanisa huko Mashariki ya Kati kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani. Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyojitokeza katika tamko la pamoja mara baada ya kuhitimisha semina iliyojadili kuhusu mchango wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa huko Mashariki ya Kati katika mchakato wa kudumisha haki na amani.

Semina hii imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Kanisa, Serikali na wadau katika sekta ya mawasiliano ya kijamii. Kwa pamoja wanasema, kuna haja kwa vyombo vya habari kulinda na kudumisha tunu za haki msingi za binadamu, amani kwa kuangalia mambo ambayo yanawagawa watu ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kudumu. Vyombo vya habari vijikite zaidi katika mchakato wa kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu badala ya kuchochea vurugu na kinzani.

Wajumbe wanasema, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vinaweza kusaidia kutunza na kuimarisha utambulisho wake, visipokuwa makini vinaweza kutumiwa na wanasiasa kwa masilahi yao binafsi, hapo utakuwa ni mwanzo wa kufilisika kwa vyombo hivi. Vyombo hivi huko Mashariki ya Kati vina dhamana nyeti ya kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Viwe ni jukwaa la majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa karibu na Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika kuchapisha vitabu na majarida mbali mbali.

Vyombo hivi viwe ni vielelezo vya msingi wa maadili na utu wema; mahali ambapo vijana wa kizazi kipya watajifunza tunu msingi za maisha ya kijamii; ili waweze kuufahamu na kuupenda ukweli; wasimame kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha; wawe ni mashahidi wa uzuri na wema unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Ni mwaliko kwa nchi zilizoko Mashariki ya Kati kusitisha vita na kinzani ambazo zimekuwa ni chanzo kikuu cha vifo na hali ngumu ya maisha na badala yake waanze mchakato wa kutetea, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na kimataifa!

Hii iwe ni fursa ya kuendeleza majadiliano ya kidugu baina ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, daima wakitafuta umoja wa kitaifa na mafao ya wengi. Watu wajifunze kuheshimiana na kuthaminiana ili kuondokana na sera tenge za kiubaguzi kwa misingi ya kidini.







All the contents on this site are copyrighted ©.