2013-06-18 08:08:42

Kuna matumaini kwa nchi 38 duniani kufikia lengo la kupambana na baa la njaa duniani!


Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limeonesha matumaini makubwa kwa nchi 38 kuweza kufikia Lengo la Kupambana na Baa la Njaa ifikapo mwaka 2015. Hii inatokana na maboresho makubwa na kipaumbele cha kwanza kuendelea kutolewa na nchi wanachama wa FAO katika sera ya kilimo na ushirikiano ili kuwa na hali bora zaidi ya chakula duniani. Sera makini za kilimo zitaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa baa la njaa duniani.

Ni maneno yaliyotolewa hivi karibuni na Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO, ambaye anaendelea kuzitaka nchi wanachama kuhakikisha kwamba, zinajifunga kibwebwe ili kutokomeza baa la njaa duniani.

Itakumbuka kwamba, Kampeni hii ya Kimataifa ilizinduliwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon kunako mwaka 2012. Kiwango cha balaa la njaa Kimataifa kimeshuka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, lakini bado kuna watu millioni 870 wanateseka kwa baa la njaa duniani na wengi wao wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha, wahanga wakuu hapa ni watoto.

Nchi 20 tayari zimeonesha kufanikiwa lengo la kwanza kati ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia la kupunguza walau nusu ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa katika nchi zao. Haya ni maendeleo yaliyopimwa kutoka mwaka 1990 hadi mwaka 1992 na Kati ya Mwaka 2012 hadi mwaka 2013, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa mwaka 2000.

Taarifa ya hali ya chakula kwa mwaka 2012 inaonesha kwamba, watu millioni 852 wanaokabiliwa na baa la njaa wanatoka katika Nchi zinazoendelea duniani. Watoto millioni 16 kutoka katika nchi hizi ambao ni asilimia 15% wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha. Baa la njaa linaendelea kuongezeka kwa kasi Barani Afrika, licha ya ukweli kwamba sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa nchi nyingi za Kiafrika, lakini bado haijapata kipaumbele cha kutosha.

Maboresho ya tija na uzalishaji ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kusaidia pia mchakato wa maboresho ya mamillioni ya watu wanaoishi vijijini; watu ambao wanategemea kilimo kama sehemu ya kipato chao cha maisha. FAO inaendelea kuzipongeza nchi mbali mbali ambazo zinaendelea kutekeleza sera ya kilimo kwanza ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora na kwamba, baa la njaa miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa itafutika kwa wakati wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.