2013-06-18 08:19:17

Kampeni dhidi ya baa la njaa duniani!


Maadhimisho ya Mkutano wa Wakuu wa G8 ilikuwa ni fursa nyingine iliyotumiwa na Makanisa nchini Uingereza kuwakumbusha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, baa la njaa ni mapambano shirikishi yanayopaswa kuanza kutimua vumbi kwenye mizizi ya tatizo ili mamillioni ya watu wasiendelee kuteseka duniani kwa kukosa chakula.

Makanisa nchini Uingereza hivi karibuni yalizundua Kampeni iliyoongozwa na kauli mbiu “Chakula cha kutosha kwa kila mtu”. Ili kuwakumbusha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, baa la njaa si mchezo, kwani kuna mamillioni ya watu wanaendelea kupotza maisha yao na kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto ambao wamekumbwa na utapiamlo wa kutisha.

Hakuna sababu msingi wanasema viongozi wa Makanisa nchini Uingereza dunia kuzalisha chakula cha kutosha na baadhi ya watu duniani wakaendelea kuteseka kutokana a baa la njaa na utapiamlo! Waamini kutoka Madhehebu mbali mbali ya Kikristo walikusanyika hivi karibuni kusali na kufunga kama kielelezo cha mshikamano wao wote wanaoteseka na baa la njaa duniani, mfumo unaoendelea kuwanufaisha watu wenye nguvu kiuchumi na kisiasa.

Huu ni mwelekeo wa kukosekana kwa misingi ya haki duniani. Baadhi ya viongozi wa Kanisa wanasema kuna wanasiasa nchini humo wameshindwa kuweka moyo wa ”nyama” katika mikakati na vipaumbele vyao kisiasa kwani wanaelemewa mno na masilahi binafsi.

Askofu Mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pian i Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani Duniani, ametumia fursa ya mkutano huu kumshukuru na kumpongeza Waziri mkuu David Cameron ambaye ameahidi kwamba, Uingereza itatenga kiasi cha asilimia 0.7% cha Bajeti yake kwa ajili ya misaada ya kimataifa kila mwaka.

Anakumbusha kwamba, G8 ni kundi kubwa lenye uwezo: kifedha na kiuchumi, likipania na kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, maendeleo makubwa yanaweza kupatikana. Hata katika nyakati za athari za myumbo wa uchumi kimataifa, bado waamini na wananchi wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Kanisa kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati unaoongozwa na Kanuni Auni, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Justin Welby kwamba, wakuu wa G8 katika mkutano wao unaohitimishwa tarehe 18 Juni 2013 wataweza kuibua mbinu mkakati wa mshikamano na nchi changa zaidi duniani. Waziri mkuu David Cameron anasema kwamba, wameisikia Kampeni ya viongozi wa kidini dhidi ya baa la njaa na wataendelea kulifanyia kazi wazo hili. Mwaka 2013 uwe ni mwanzo wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.









All the contents on this site are copyrighted ©.