2013-06-18 08:38:08

Jifunzeni kuhifadhi misitu na kutunza vyanzo vya maji ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula!


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 17 Juni inaadhimisha Siku ya Kupambana na Jangwa na Ukame Duniani. Mwaka huu kampeni kubwa inapania kuwasaidia wananchi kutambua athari zinazotokana na ukame na ukosefu wa maji. Gharama yake ni kibwa katika maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hili ni tatizo ambalo linaikumba dunia nzima na hakuna nchi ambayo inaweza kujigamba kwamba, iko salama.

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, dunia inaonekana kwamba, imeelemewa na ukame ambao kwa sasa linaonekana kana kwamba, ni jambo la kawaida hasa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya siku hii anabainisha kwamba, ukame wa muda mrefu una madhara makubwa katika maisha ya watu.

Hili ni tatizo linalopaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa pamoja; kabla na wakati. Wananchi wafundishwe njia za kupambana na jangwa pamoja na kuwa na mikakati madhubuti itakayowasaidia kutunza vyema vyanzo vya maji. Jamii ijifunze kutunza ardhi kwa vitendo kama ambavyo wajumbe wa mkutano wa Maendeleo endelevu uliofanyika Rio de Janeiro ulivyokazia. Kwa kutunza vyema misitu na vyanzo vya maji, jamii itakuwa inajionegezea uwezo wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakala, lishe bora pamoja na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi.







All the contents on this site are copyrighted ©.