2013-06-17 08:20:25

Siku ya Mtoto wa Afrika Tanzania


Hotuba ya mhe. Sophia M. Simba (mb), Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto wakati akizindua rasmi mtandao wa mawasiliano ya simu wa kusaidia watoto hapa nchini (Tanzanian child helpline) tarehe 16 Juni, 2013.

Kwanza, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha sote kukutana hapa ili kuweza kushuhudia tukio hili muhimu katika kuwezesha watoto kupata mojawapo ya haki yao ya msingi.

Ndugu Wageni Waalikwa

Mnamo mwaka 2009 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya watoto hapa nchini ilifanya utafiti wa kina ili kufahamu ukubwa na sura ya ukatili wa kijinsia, kimwili na kiakili yanayowasibu wasichana na wavulana hapa nchini.

Utafiti huu ulifanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi na Tiba cha Muhimbili (Muhimbili University of Health and Allied Sciences – MUHAS) kwa kushirikiana na UNICEF na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Center for Diseases Control – CDC). Ripoti ya Utafiti huu ilizinduliwa rasmi mnamo tarehe 09 Agosti, 2011 na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bibi Asha-Rose Migiro.

Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa kuna kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto na matukio mengi ya ukatili kwa watoto yamekuwa yakifanyika ama shuleni na au nyumbani. Hali hii ilipelekea wadau wa masuala ya watoto (Taasisi za serikali na zile zisizokuwa za serikali) kuandaa Mpango Mkakati wa mwaka mmoja wa Kushughulikia Tatizo la Ukatili Dhidi ya Watoto (2012 – 2013) na hatimaye kuandaa Mpango wa miaka mitatu wa kushughulikia tatizo hilo (2013 – 2016) ambao ulizinduliwa mwezi April mwaka huu.

Ndugu Wageni Waalikwa.

Mnamo tarehe 3 Januari, 2013 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliingia makubaliano na Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali ya C-Sema kuhusu uendeshaji wa mtandao huu katika maeneo ya majaribio (Pilot Areas). Uendeshaji wa mtandao huu katika maeneo haya utasaidia kutoa picha halisi ya namna nzuri ya uendeshaji wa mtandao wa namna hii hapa nchini. Mtandao huu utafanya kazi katika Wilaya/ Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu na Hai ambapo muda si mrefu utaanza kufanya kazi katika Manispaa za Ilala na Kinondoni. Lengo kuu la Serikali kwa kushirikiana na wadau wake wa maendeleo ya watoto ni kuhakikisha kuwa mtandao huu unafanya kazi katika maeneo yote ya Tanzania Bara.

Ndugu Wageni Waalikwa
Uanzishaji wa Mtandao wa Mawasiliano wa Kusaidia Watoto ni moja wapo ya shughuli ambazo zilipangwa kutekelezwa na Wizara yangu katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Kushughulikia Ukatili Dhidi ya Watoto uliozinduliwa hivi karibuni. Kadhalika, ni moja wapo ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watoto (The UN Convention on the Rights of the Child – UN CRC) ambao nchi yetu iliusaini na kuuridhia mara baada ya kupitishwa kwake.

Mtandao huu utatoa fursa kwa watoto na au watu wazima kwa niaba ya watoto kutoa taarifa za ukatili unaofanywa kwa watoto katika eneo fulani ili kuwezesha wahusika kufuatilia kwa karibu na urahisi kwa ajili ya kutoa msaada kwa mtoto/watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili na kumchukulia/kuwachukulia hatua mhusika/wahusika wa vitendo hivyo vya ukatili.

Kwa kiasi kikubwa kama mtandao utatumiwa kwa malengo haya, ni imani yangu kuwa itasaidia kupunguza ukatili dhidi ya watoto na vile vile kuhakikisha kuwa watoto wanapata msaada stahiki kwa wakati.

Ndugu Wageni Waalikwa
Ni matumaini ya Wizara yangu kuwa wadau mbalimbali watajitokeza kushirikiana nasi katika kuhakikisha kuwa huduma hii inapatikana katika maeneo yote hapa nchini katika muda muafaka ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata ulinzi wa kutosha.

Kadhalika, ni matumaini yangu kuwa jamii na wahusika wote watawezeshwa kupata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi sahihi ya mtandao huu.

Mwisho, napenda pia kuchukua fursa hii rasmi kutamka kuwa nimezindua rasmi mtandao wa mawasiliano ya simu wa kusaidia watoto katika maeneo ya majaribio niliyoyataja hapo mwanzo.

Tuungane kwa Pamoja Kuijenga Tanzania Imfaayo Mtoto.

Asanteni Sana kwa Kunisikiliza








All the contents on this site are copyrighted ©.