Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika yakoleze mapambano dhidi ya mila na desturi zilizopitwa
na wakati!
Shirika la kuhudumiwa watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF katika Maadhimisho ya Mtoto
wa Afrika yaliyofikia kilele chake hapo tarehe 16 Juni 2013, linasema kwamba, kuna
nchi kumi Barani Afrika ambazo bado kiwango cha vifo vya watoto wenye umri chini ya
miaka mitano kiko juu zaidi. Nchi hizi ni pamoja Sierra Leone, Mali, Chad, DRC, Jamhuri
ya Watu wa Afrika ya Kati, Guinea Bissau, Angola, Burkina Faso na Burundi.
UNICEF
inapenda kushirikiana kwa karibu zaidi na Umoja wa Afrika ili kuhakikisha kwamba,
mila zote zenye kuleta madhara kwa watoto zinaondolewa kwani hili ni jukumu la kila
mmoja. Itakumbukwa kwamba, hii ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza pia Maadhimisho ya
Siku ya Mtoto wa Afrika kwa Mwaka 2013.
Familia na Jamii kwa ujumla ni msingi
wa ustawi, maendeleo na afya bora kwa watoto Barani Afrika. Kuna haja ya kuhakikisha
kwamba, mila za ukeketaji kwa watoto wa kike zinapigwa marufu. Bado kuna ndoa za utotoni
katika baadhi ya nchi za Kiafrika vitendo vinavyodumaza maisha ya watoto wengi.
Kati
ya mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga UNICEF inasema, ni watoto kuhusishwa na imani
za kishirikina jambo ambalo limepelekea watoto wengi kutolewa sadaka kwa kudhani kwamba,
ni chambo cha fedha, utajiri na madaraka. Ni katika mwelekeo kama huu, watoto na watu
wenye ulemavu wa ngozi wamejikuta wakidhulumiwa katika Jamii.