Dini zinawajibu wa kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu!
Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, Jumamosi
jioni tarehe 15 Juni 2013 ameshiriki katika Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Ceadda, London, Uingereza. Amekazia umuhimu wa kulinda. Kudumisha
na kutetea utu na heshima ya kila mtu kama kielelezo makini cha ujenzi wa misingi
ya haki na amani duniani.
Kardinali Tauran ameyasema haya wakati wa ziara
yake ya kichungaji nchini Uingereza kama sehemu ya mchakato unaopania kujenga na kuimarisha
urafiki kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani, ziara ambayo ilianza rasmi hapo
tarehe 12 na kuhitimishwa hapo tarehe 16 Juni 2013.
Akiwa mjini London, Kardinali
Tauran amekuta na kuzungumza na waamini wa dini mbali mbali nchini Uingereza pamoja
na kushiriki sala kwa ajili ya kuombea misingi ya haki na amani, iliyowashirikisha
waamini wa dini mbali mbali duniani. Katika mahubiri na hotuba zake, amekazia umuhimu
wa kujenga na kuimarisha amani.
Wakati wa machafuko, kinzani na migogoro mambo
ambayo yanapelekea kuvunjika kwa misingi ya amani, watu wengi wanajikuta wakiteseka
na kuhangaika kutokana na baadhi ya watu kutafuta masilahi yao binafsi badala ya kuchuchumilia
mafao na ustawi wa Jamii inayohusika. Kutokana na kuwepo kwa wasi wasi wa kutokomea
kwa misingi ya amani, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuzungumzia suala
hili, na kila mmoja ajitahidi kuwa kweli ni chombo cha amani pamoja na kushikamana
na watu wengine kwa ajili ya mafao ya wengi.
Kardinali Tauran anasema kwamba,
dhana ya jirani imekuwa na kupanuka kutokana na utandawazi na mwingiliano wa watu
wanaohama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Hawa ni watu wenye imani, tamaduni na
asili tofauti; kimsingi ndio wanaounda kundi la majirani, changamoto ya kujenga urafiki
na wote; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kushirikiana pamoja na kusimama kidete
kulinda na kutetea haki na mafao ya wengi; amani na utulivu pamoja na maendeleo endelevu.
Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushirikiana katika kuenzi tunu msingi
za maisha ya kijamii kama nguzo za ujenzi wa amani.