Wakristo wanahamasishwa kuwa ni wajumbe wa amani na upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu!
Maisha ya Kikristo si mwaliko kwa waamini kujitafuta na kujitafutia amani yao binafsi,
bali wanatumwa na Kristo kwenda hadi miisho ya dunia kutangaza Habari Njema ya Wokovu
na kwamba, Yesu amejinyenyekesha ili aweze kuwa ni daraja ya upatanisho kati ya Mungu
na mwanadamu.
Yesu Kristo ameonesha utii, hata akahesabiwa kuwa ni kati ya
wadhambi ili kumpatanisha mwanadamu na Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini
kuhakikisha kwamba, wanajipatanisha na Mungu kama wanavyohamasishwa na Mtakatifu Petro
katika Waraka wake kwa Wakorintho. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 15 Juni 2013 wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya
Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican.
Upatanisho
ni mchakato ambao umemfanya Yesu Kristo kujitwika dhambi za binadamu, ili aweze kuwapatanisha
na Mwenyezi Mungu na hivyo kuwajalia Sakramenti ya Upatanisho inayomwonjesha mwamini
huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Waamini wanapomuungamia Yesu dhambi
zao, anawasamehe na kuwapatia mwelekeo mpya wa maisha kwani hii ni sehemu ya utume
wake hapa duniani, uliopelekea hata akateswa, kufa na kufufuka kutoka katika wafu.
Waamini waonje na kuguswa na upendo wa Kristo ndani mwao!
Baba Mtakatifu anasema,
amani mintarafu Mafundisho ya Kristo ni mchakato unaowasukuma waamini kupeleka ujumbe
wa upatanisho kati ya Mungu na binadamu hadi miisho ya dunia, huku wakihamasishwa
na utume huu ambao wamekabidhiwa na Kristo mwenyewe na kiini cha utume wao! Waamini
wanapaswa kulifahamu Fumbo la Msalaba katika maisha yao, Msalaba ambao ni matokeo
ya dhambi na uasi wa binadamu.
Huu ni ukweli unaofumbatwa katika Fumbo la
Msalaba, pale ambapo moyo wa Yesu Kristo ulipotobolewa kwa mkuki, humo yakatoka maji
na damu; kielelezo cha Sakramenti za Kanisa. Hapa ni mahali ambapo hekima ya Kikristo
ikabubujika na kwamba, amani ya kikristo inafumbatwa katika uhalisia wa maisha na
kwamba, upendo wa Kristo unawawajibisha kutangaza ujumbe wa amani na upatanisho miongoni
mwa watu!