2013-06-14 15:01:38

Wajaini na Wakatoliki wanachangamotishwa kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu!


Kwa mara ya kwanza Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini lilianza kushirikiana kwa karibu zaidi na waamini wa dini ya Kijaini kunako mwaka 1986 wakati wajumbe wa dini hii waliposhiriki pamoja na viongozi wengine wa dunia kusali kwa ajili ya kuombea amani, tukio ambalo lilihitishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Tangu wakati huo waamini hawa wameendelea kushirikiana na Makanisa mahalia pamoja na mikutano na matukio mbali mbali yaliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini.

Wajaini na Wakatoliki wanahamasishwa kushikamana kwa ajili ya kulinda na kutetea misingi ya haki, amani upendo na mshikamano miongoni mwa Jamii. Yesu aliteswa na kufa Msalabani, lakini daima amekuwa ni kielelezo cha haki, amani na mapendo kati ya watu hasa kutokana na mafundisho yake yanayohimiza upendo kwa Mungu na jirani. Fadhila hii inapatikana pia miongoni mwa wafuasi wa dini ya Jaini.

Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa Ijumaa tarehe 14 Juni 2013 na Kardinali Jean Lous Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini alipokutana na kuzungumza na viongozi na baadhi ya waamini wa dini ya Jaini, Jijini London. Fadhila hii inawachangamotisha waamini wa dini hizi mbili kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, licha ya tofauti zao za kiimani. Wanaalikwa kuchangia mchakato wa kudumisha upendo, haki, amani, uhuru, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu katika ujumla wake.

Kardinali Tauran anasikitika kusema kwamba, kuna hatari kubwa inayoendelea kujitokeza kwani mara nyingi waamini wanashindwa kumwilisha kanuni na misingi ya dini zao na matokeo yake wamekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kidini kutokana na misimamo mikali ya kiimani, hali ambayo imepelekea hata uvunjifu wa misingi ya haki na amani sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mtaji huu watu wanashindwa kuona tena maana na mchango wa dini katika maisha, ustawi na maendeleo ya watu.

Kardinali Tauran anakumbusha kwamba, kimsingi dini ya kweli ni chanzo kikuu cha upendo, umoja na mshikamano wa kweli, kinyume chake ni watu kujitafuta wenyewe na mafao yao kwa kutumia mgongo wa dini, jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya mwanadamu. Kuna watu ambao ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani duniani, hawa ni pamoja na Mahatma Gandhi pamoja na Martin Luther King, ni watu ambao hawakutumia nguvu wala mabavu, lakini wamechangia kwa kiasi kikubwa mchakato wa amani na utulivu kati ya Jamii.

Papa Paulo wa sita alikwishawahi kuwachangamotisha Wakristo kuachana kabisa na mambo yote yanayoleta madhara katika uhai, utu na heshima ya binadamu na badala yake wakumbatie na kuenzi misingi ya haki na amani na udugu wa upendo. Kanisa linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushinda ubaya kwa kutenda mema.

Ni matumaini ya viongozi wa kidini kwamba, watachangia kwa kina na mapana mchakato wa kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano; daima wapanie kukoleza majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wao. Changamoto hii itekelezwe kwa mawazo, maneno na matendo kwa kuonesha huruma na upendo; wema na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.