2013-06-14 09:36:17

Makanisa nchini Uganda ni sauti ya kinabii inayotetea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano


Uganda ni kati ya nchi za Kiafrika ambazo zimeshuhudia damu ya watu wake wasiokuwa na hatia ikimwagika. Ni nchi ambayo imeonja athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kinzani za kisiasa, kijamii na kidini. Yote haya yamepelekea Makanisa nchini Uganda kushikamana kwa pamoja ili kulinda, kutetea sanjari na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; utu na heshima ya mwanadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Ni mchango wa Mchungaji Grace Kaiso, Katibu mkuu wa Majimbo ya Kanisa Anglikani Barani Afrika katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika lilipoanzishwa. Anasema, kuna viongozi wa Kanisa kama vile Askofu mkuu Janan Luwum aliyehoji kuhusu mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na utekaji nyara uliokuwa unafanywa na utawala wa Id Amini kunako mwaka 1977. Hata hivyo bado rushwa, ufisadi na kinzani za kivita na kisiasa na kijamii zimeendelea kushamiri sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Makanisa kwa namna ya pekee kabisa yamejitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanadamu hata kwa gharama ya maisha yao. Yako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya baa la umaskini, ujinga na maradhi na kwamba, ni wadau wakuu wanaotetea haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.

Mchungaji Grace Kaiso anasema, Kanisa la Uganda limekumbana na changamoto zote hizi, lakini limeendelea kutoa mchango wake wa hali na mali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Uganda katika ujumla wake. Umefika wakati kwa Makanisa Barani Afrika kupiga hatua mbele kwa kujihusisha zaidi na zaidi katika kuponya madonda ya vita, chuki na utengano kwa ajili ya kuimarisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Kanisa liko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ukimwi, Uharibifu wa mazingira na masuala ya usawa kati ya wanaume na wanawake wanaopaswa kukamilishana. Hii ndiyo sauti ya kinabii inayotolewa na Makanisa nchini Uganda. Wanawake na vijana wanapaswa kushirikishwa zaidi katika ujenzi na ustawi wa nchi yao na kwamba, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa sana kwa Kanisa katika kudumisha misingi ya haki, amani na utu wa mtu.







All the contents on this site are copyrighted ©.