2013-06-14 09:09:28

Caritas inapenda kumwonjesha mwanadamu huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya huduma makini!


Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni mada ambayo inaendelea kupewa msukumo wa pekee katika Makanisa mahalia ili kuliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu utakaowawezesha watu wengi kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi.

Changamoto hii inafanyiwa kazi na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini lililoanza mkutano wake hapo tarehe 9 na unatarajiwa kukamilika tarehe 16 Juni 2013. Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum katika Ibada ya ufunguzi wa mkutano huu amekazia kwa namna ya pekee nguvu ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Wajumbe wanapembua kwa kina kuhusu: utambulisho wao, tasaufi na utume wa Caritas kwenye Ukanda wa Amerika ya Kusini kwa kutambua usawa kati ya wanawake na wanaume katika kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zao.

Caritas inapenda kutumia tafiti na sera mbali mbali katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na maradhi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini wanapaswa kuhudumiwa kwa haraka na vyema zaidi kwani hawana tena muda wa kusubiri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna mamillioni ya watu duniani yanaendelea kuteseka kutokana na baa la njaa, wakati ambapo kuna watu wanakula na kusaza hadi kutupa chakula!

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alisema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na athari kubwa za myumbo wa uchumi, kimaadili, kitamaduni na kiimani. Madhara yake yanajionesha katika maisha ya mwanadamu. Kuna haja ya kutambua na kuheshimu utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hata katika hali ya ugonjwa na umaskini wake.

Caritas inapenda kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwa njia ya huduma makini.







All the contents on this site are copyrighted ©.