2013-06-13 15:19:53

Wapendeni na kuwaheshimu jirani zenu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Mathae mjini Vatican siku ya Alhamisi, amekazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana miongoni mwa waamini kama njia ya kutekeleza shughuli ya Uinjilishaji.

Ni mwaliko wa kuheshimiana na kuthaminiana katika hija ya maisha ya hapa duniani, kama Kristo mwenyewe alivyojinyenyekeza akawa mtii hata kufa Msalabani, kiasi cha kuwajalia wafuasi wake ile dhamana ya kuwa ni ndugu zake wapendwa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutumia vyema ndimi zao, kwani ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili wa mwanadamu, lakini kinaweza kusababisha madhara makubwa katika maisha ya watu. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu amemwekea mwanadamu amri ya kutosema uongo, ili kujengana na kuimarishana katika mambo mema. Waamini wajenge fadhila ya unyenyekevu, wakiongozwa na sheria ya upendo kwa Mungu na jirani; wasimame kidete kulinda na kutetea haki na amani.

Baba Mtakatifu amewapongeza wananchi wa Argentina wanaoishi na kufanya kazi zao hapa mjini Roma kutokana na mchango wao kwa maendeleo na ustawi wa Argentina. Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na Balozi wa Argentina nchini Italia ambaye pia ni mwakilishi wa FAO.

Papa anawataka waamini kuendelea kujishikamanisha na sheria ya Mungu ambayo Kristo mwenyewe ameipatia utimilifu wake. Ili kujenga na kuimarisha mahusiano mema, kuna haja kwa waamini kuendelea kufanya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawalika waamini kuwapenda na kuwaheshimu jirani zao, kwa kuwatakia mema!







All the contents on this site are copyrighted ©.