2013-06-13 15:18:38

Sinodi za Maaskofu ni chombo makini katika maisha na utume wa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza, Alhamisi, tarehe 13 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya Sinodi ya Kumi na tatu ya Maaskofu, kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; dhamana inayohitaji utayari, uwajibikaji na sadaka ambayo wakati mwingine inawalazimisha kusafiri umbali mrefu.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaopania kutangaza imani ya Kikristo na kwamba, hii ndiyo dhamana ya Kanisa kwa ujumla, hususan katika nchi ambazo zilibahatika kusikia Injili ya Kristo lakini kwa sasa zimemezwa na malimwengu. Waamini katika nchi hizi wanapaswa kutangaziwa Injili ili waweze kukutana tena na Kristo anayewakirimia mabadiliko mapya katika hija ya maisha yao ya ndani kabisa. Hii ni changamoto ya mikakati ya kichungaji.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kuna haja ya kuibua mbinu na mikakati mipya kutokana na mabadiliko yanayoendelea kujitokeza kwenye Jamii nyingi pamoja na kupambanua mbinu ambazo Mama Kanisa anaweza kuzitumia ili kufikisha ujumbe wa Injili ya Kristo kwa watu nyakati hizi sanjari na kupata majibu makini ya masuala yanayomtatiza binadamu ili kuimarisha mshikamano wa dhati, kama alivyowahi kubainisha Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa sita.

Dhamana ya Uinjilishaji si tu kwa ajili ya Wakristo bali ni kwa ajili ya binadamu wote, changamoto anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini wote kujisikia kuwa ni wadau wa Uinjilishaji Mpya, na kamwe wasiogope kutoka katika ubinafsi wao huku wakijiaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu unaowaongoza, bila kusahau kwamba, Mwinjilishaji Mkuu ni Roho Mtakatifu anayesaidiwa na vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii.

Waamini wanapaswa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu awasaidie kutoa ushuhuda wa Injili unaomwilishwa kwa njia ya matendo, moyo wa sala, upendo kwa wote, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; Unyenyekevu na moyo wa kiasi na zaidi sana, utakatifu wa maisha! Kwa njia hii, Uinjilishaji utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Sinodi za Maaskofu ni kati ya matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, katika kipindi cha miaka hamsini, zimekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu, hali ambayo ameishuhudia mwenyewe wakati alipokuwa anahudhuria Sinodi mbali mbali. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Sinodi za Maaskofu zitaendelea kuboreshwa ili kuimarisha majadiliano na ushirikiano miongoni mwa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe kwa mkutano wao uliomsaidia kuweza kubaini tema itakayoongoza Sinodi nyingine tena ya Maaskofu. Amewashukuru wote kwa moyo wa ukarimu, utayari na ushirikiano waliomwonesha na kwamba, kazi hii kwa wakati muafaka itaweza kuzaa matunda ajaa kwani Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima kwa kila mtu na kila mmoja wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.