Simameni kidete kulinda, kutetea na kuendeleza misingi ya haki, amani na mshikamano!
Kardinali Jean Lous Tauran wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Uingereza, siku ya
Alhamisi tarehe 13 Juni 2013 alitembelea Seminari ya dini ya Kihindu. Katika hotuba
yake amekazia kwa namna ya pekee, ushirikiano unaopaswa kujengeka kati ya waamini
wa Kanisa Katoliki na Wahindu katika kujenga na kuimarisha utamaduni wa kujali kama
msingi wa ujenzi wa amani. Kanisa Katoliki linapania kuendeleza ushirikiano na waamini
wa dini ya Kihindu mahali popote pale walipo.
Katika ulimwengu wa utandawazi,
mapokeo ya dini nyingi yanaonekana kana kwamba, yamepotea na kumezwa na malimwengu.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican miaka hamsini iliyopita, walikazia umuhimu
wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani; changamoto hii inapaswa
kufanyiwa kazi hasa wakati huu ambapo kuna mwingiliano mkubwa wa watu wenye dini na
tamaduni mbali mbali.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alipokutana
kwa mara ya kwanza na wawakilishi wa dini na madhehebu mbali mbali waliokuwa wamehudhuria
Ibada ya Misa Takatifu wakati alipokuwa anasimikwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro,
alisema, Kanisa Katoliki linatambua umuhimu wa kudumisha urafiki, heshima miongoni
mwa Jamii ya watu wenye dini na mapokeo mbali mbali ni dhamana ambayo imeendelezwa
kwa namna ya pekee na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini tangu lilipoanzishwa.
Hii ni changamoto kwa waamini kujitahidi kufahamu imani ya jirani zao; waguswe
na hekima na wema unaopatikana kwenye dini hizi sanjari na kuunda mazingira yatakayowawezesha
watu wote kuishi kwa amani, uhuru na utulivu. Mchakato huu uwasaidie waamini wa dini
mbali mbali kuwa kweli ni wachamungu. Huruma ni fadhila inayopatikana katika dini
mbali mbali duniani kama ilivyobainishwa katika Vitabu Vitakatifu, kiasi cha kuwawezesha
watu kama akina Mahatima Ghandi wakasimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki
na amani.
Kardinali Tauran anasema fadhila ya huruma iwasaidie waamini kuguswa
na mateso ya jirani zao, kiasi cha kushiriki kuleta mabadiliko katika ulimwengu mamboleo,
kama alivyofanya yule Msamaria mwema anayesimuliwa katika Maandiko Matakatifu. Baba
Mtakatifu Francisko katika utume wake anaendelea kuwahamasisha wakristo na watu wote
wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa dhati na maskini na wote wanaoteseka sehemu
mbali mbali za dunia.
Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kuonesha
umuhimu kwa Jamii kushirikiana na kushikamana ili kwa pamoja waweze kukabiliana na
changamoto hizi, kwa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani, licha ya tofauti
za kiimani. Lakini anasema Kardinali Tauran fadhila ya huruma inawaunganisha wote
mintarafu Mapokeo ya dini zao, changamoto na mwaliko wa kukua na kukomaa katika maelewano,
kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda, kutetea
na kuendeleza misingi ya: haki, amani na mshikamano.