2013-06-13 10:48:11

Njia za mawasiliano ya jamii ni upanga wenye makali kuwili!


Wadau wa mawasiliano ya jamii ni mashahidi wa wema, ukweli na mambo mazuri ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko alipokutana kwa mara ya kwanza ya waandishi wa habari mjini Vatican mara baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni watu wenye mchango mkubwa katika huduma kwa haki na amani pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Njia za mawasiliano ya Jamii ni jambo muhimu sana katika kukuza na kuendeleza ushirikiano na mshikamano kati ya watu wanaotoka katika medani mbali mbali za maisha. Vyombo vya mawasiliano ya Jamii vina nguvu ya kuweza kuimarisha Serikali madarakani, lakini pia ni upanga wenye makali kuwili, unaoweza kuvifanya vyombo vya habari kuwa ni chanzo cha vita, vurugu na kinzani za kijamii; vina uwezo wa kuwainua baadhi ya watu ndani ya Jamii na kuwabeza wengine kiasi cha kuonekana si watu tena bali viatu!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem, wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kwa kushirikiana na Kituo cha Kikatoliki cha Masomo na Mawasiliano mjini Amman. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu "Vyombo vya Kikristo vya Kiarabu katika huduma ya haki, amani na haki za binadamu". Mkutano huu umehudhuriwa na Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii pamoja na viongozi wengine wa Kanisa na Serikali kutoka Yordan.

Ni matumaini ya Patriaki Twal kwamba, nchi ya Yordan itaendelea kubaki kuwa ni kielelezo cha upendo na umoja wa kitaifa na kwamba, Wakristo kutoka katika nchi za Kiarabu wataendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi zao kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Kanisa kwa upande wake litaendelea kuchangia pia katika sekta ya elimu. Vyombo vya habari havina budi kuwa ni chemchemi ya uhuru, ukweli na uwazi; uchaji wa Mungu; Maadili na Utu wema. Haya ni mambo msingi yanayounda misingi ya imani.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji Kanisa Mashariki ya Kati anawaalika waamini kujenga na kuimarisha umoja na ushuhuda wa maisha; daima wakishiriki katika ujenzi na ustawi wa nchii zao na kamwe wasiwe ni raia daraja la pili. Kila raia achangie ustawi wa nchi yake kadiri ya uwezo wake.

Lugha ya Kiarabu kwa sasa inatumiwa na Vatican katika nyaraka zake mbali mbali ili kuwawezesha wananchi kutoka katika nchi za Kiarabu kupata ujumbe huo katika lugha yao wenyewe!

Vyombo vya habari vya Kikristo vinaweza kuchangia kwa kina na mapana katika ustawi na maendeleo ya watu wao; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea vipaumbele vya kijamii, utu na heshima ya watu wanaowahudumia.







All the contents on this site are copyrighted ©.