Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto kwa waamini kusimama kidete kulinda na
kutetea Injili ya Uhai, kwani ni kwa njia ya kuamini, waamini wanaweza kupata maisha
tele! Ni changamoto endelevu inayotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland mara
baada ya kuhitimisha mkutano wao wa mwaka hivi karibuni.
Maaskofu wanawaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za
Mama Kanisa katika kulinda na kutetea Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa
mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo kinapomfika kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu.
Kwa namna ya pekee, Mama Kanisa ataadhimisha tukio hili mjini Vatican kwa kuungana
na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 15 na kilele chake kitakuwa katika
Ibada ya Misa Takatifu Jumapili, tarehe 16 Juni 2013 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican.
Kauli mbiu iliyochaguliwa katika Maadhimisho haya inaonesha
jinsi ambavyo Kanisa linapania kulinda na kudumisha utu, heshima na maisha ya binadamu.
Ibada hii ni kwa ajili ya kuenzi wale wote ambao wanapenda kuunga mkono juhudi za
Kanisa katika kutetea na kutangaza Injili ya uhai, kama alivyofanya Mwenyeheri Yohane
Paulo wa pili kunako tarehe 25 Machi 1995 alipochapisha Waraka wa Kichungaji, Injili
ya Uhai, dira na mwongozo kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kupinga kwa nguvu
zao utamaduni wa kifo!
Baraza la Maaskofu nchini Ireland limeonesha nia na
utashi wa kuendeleza huduma ya hali na mali pamoja na utoaji wa ushauri nasaha kwa
wale walioathirika kutokana na nyanyaso za kijinsia walizofanyiwa na baadhi ya viongozi
wa Kanisa, kama njia ya kukuza na kudumisha haki.
Maaskofu wa Ireland wanapenda
kuwakaribisha viongozi wa G8 watakaofanya mkutano wao mkuu hapo tarehe 17 hadi 18
Juni 2013 mjini Enniskillen, kwa kuwataka kutambua na kuthamini mshikamano wa kimataifa
unaoongozwa na kanuni auni kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na hali ngumu ya
uchumi duniani; magonjwa, ujinga na baa la njaa linaloendelea kuwakumba maelfu ya
watu duniani.
Wananchi wengi wamekata tamaa kutokana na hali ngumu ya maisha
wanayokabiliana nayo, kumbe, kuna haja kwa viongozi wa G8 kuibua mbinu mkakati utakaosaidia
kuwajengea tena wananchi matumaini katika maisha yao. Wamekazia ukweli na uwazi katika
masuala ya fedha na kodi na kwamba, nchi maskini wanapaswa kufaidika na utajiri wa
rasilimali za nchi zao kwani hii ni haki yao msingi.
Maaskofu wanasema kwamba,
ni kashfa kubwa kwa sasa kuona watu wanaendelea kuteseka kutokana na baa la njaa na
utapiamlo wa kutisha wakati dunia imeonesha mabadiliko na maendeleo makubwa katika
ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana
kufa na kupona ili kurekebisha mifumo tenge inayoendelea kusababisha ukosefu wa haki
msingi duniani.
Viongozi wa Kimataifa wanapaswa pia kutekeleza ahadi zao ili
kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia Kimataifa ifikapo mwaka 2015. Mageuzi
ya biashara na soko la kimataifa; udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi na
matumizi mabaya ya nishati uoto ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa kwa ukweli
na uwazi ili kujenga na kudumisha haki jamii, amani na mshikamano wa kimataifa.
Baraza
la Maaskofu Katoliki linaendelea kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 itakayofanyika mjini Rio de Janeiro
kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu "basi enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi". Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu
la Dublin ataongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu unaowajumuisha vijana 165 kwenda
kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Vijana watakaobaki nchini Ireland watafanya
maadhimisho kwenye Majimbo yao kadiri ilivyopangwa.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Ireland limefanya kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Maadhimisho ya Kongamano la 50
la Ekaristi Takatifu Kimataifa lilipoadhimishwa mjini Dublin na kwamba, walipata nafasi
ya kutafakari kwa mara nyingine tena nyaraka za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Maaskofu wanawashukuru
sana waamini na watu wenye mapenzi mema waliochangia kwa hali na mali ili kufanikisha
tukio hili la kiimani. Maaskofu wanawaalika waamini kufanya uchambuzi yakinifu ili
kubainisha urithi unaojikita katika Maadhimisho ya Kongamano la 50 la Ekaristi Takatifu
Kimataifa.
Mwishoni, Maaskofu wamezungumzia kuhusu mgogoro wa Syria na athari
zake na kwamba, wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na wale wote walioguswa
na vita inayoendelea nchini humo. Wamekazia umuhimu wa Sakramenti ya ndoa na Familia
katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hii ni mada itakayofanyiwa kazi mwezi
septemba mwaka huu.