Watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi ni matokeo ya biashara haramu ya binadamu!
Biashara haramu ya binadamu ni kati ya sababu kubwa zinazopelekea watoto wengi kujikuta
wanaoishi katika mazingira hatarishi na matokeo yake wanakumbana na nyanyaso na madhulumu
ya kila aina. Ni watoto ambao wanaathirika tangu wakiwa wadogo na hivyo kuwa ni tishio
kwa Jamii kwa siku za usoni.
Kuna baadhi ya watoto ambao kutokana na kumong'onyoka
kwa misingi ya maadili na utu wema, wakajikuta wakiacha masomo kutokana na sababu
mbali mbali na matokeo yake sasa wanaishi kwenye mazingira magumu, licha ya wazazi
na walezi wao kuwapatia fursa ya kusoma.
Haya ndiyo yanayoendelea kujitokeza
nchini Sierra Leone, Afrika Magharibi, ambako biashara haramu ya binadamu inafanywa
hata na ndugu na jamaa wa karibu kwa madai kwamba watakapofika mjini watawapatia elimu
bora na ajira itakayowajengea uwezo wa kusaidia familia zao kijijini. Lakini wanapofika
mjini Freetown, mambo yanabadilika na kujikuta wanafanyishwa kazi kama watumwa majumbani
au kutumbukizwa na kutekelezwa kwenye biashara haramu ya ngono.
Uchunguzi wa
kina uliofanywa kunako mwaka 2010 unaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto 2,500 wanaolala
kwenye mitaa ya Mji wa Freetown kila siku, hali inayopelekea nyanyaso na madhulumu
kwa watoto hao. Ni mashirika machache yasiyo ya Kiserikali ambayo yameanzisha mchakato
wa kuwakusanya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwarudisha kwenye
familia zao, jambo ambalo si rahisi hata kidogo. Kuna haja kwa Jamii kusimama kidete
kulinda na kutunza utu na heshima ya watoto hawa!