2013-06-12 14:45:36

Waamini wanachangamotishwa kukumbatia sheria ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake siku ya Jumatano tarehe 12 Juni 2013 asubuhi kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, amewataka waamini kukua na kukomaa katika sheria ya Mungu inayojikita katika moyo wa mwanadamu, kwa kusikiliza kwa makini mafundisho ya Yesu, ili kujenga moyo wa ibada na uchaji wa Mungu. Waamini wajifunze kuwa huru mbele ya Roho Mtakatifu anayewakirimia uhuru mkamilifu zaidi.

Waamini watambue kwamba, wanaweza kupata uhakika wa usalama wao kwa kukimbilia kwa Roho Mtakatifu anayewajalia ujasiri na moyo wa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi katika mchakato wa kumwilisha Neno la Mungu katika ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu wa utandawazi kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni na sheria, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanakumbatia mambo msingi ya maisha, vinginevyo wanaweza kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Kuna vishawishi vingi, lakini waamini wawe makini kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na sheria ya Mungu ambayo imeandikwa katika mioyo yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.