2013-06-12 08:46:01

Waamini wa Kanisa Katoliki katika Nchi za Falme za Kiarabu wanaendelea kuimarika katika imani na Makanisa kuongezeka!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, yuko kwenye ziara ya kichungaji kwenye Nchi za Falme za Kiarabu na anatarajiwa kuhitimisha ziara hii, Jumamosi tarehe 15 Juni 2013. Akiwa kwenye nchi hizi atakutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, Mapadre, Watawa na Waamini kwa ujumla.

Kardinali Filoni, Jumatano tarehe 12 Juni 2013 ametembelea Msikiti mkubwa wa Sheikh Zayed ulioko Abu Dhabi pamoja na Shule ya Mtakatifu Yosefu inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, kielelezo makini cha mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu.

Kilele cha ziara hii ni hapo tarehe 14 Juni 2013, Kardinali atakapotabaruku Kanisa la Mtakatifu Antoni wa Padua lililojengwa kwa nguvu ya waamini wanaofanya kazi kwenye Falme za Kiarabu; watu ambao wana imani thabiti hata wanapokuwa ugenini. Wakristo wanaendelea kupata nafasi ya kujenga Makanisa kutokana na ushirikiano mwema kati ya viongozi wa Kanisa na Serikali ya Falme za Kiarabu; mchango mkubwa ulioanza kutekelezwa kunako mwaka 2007 mara baada ya Falme za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.