2013-06-12 14:37:32

Ole wao wanaozima cheche za matumaini na furaha miongoni mwa watoto!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Kanisa kama Familia ya Mungu amekumbusha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa tarehe 12 Juni 2013 inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupambana na kazi za suluba kwa watoto wadogo hasa wale wanaofanyishwa kazi za majumbani.

Hili ni jambo ambalo linaongezeka siku hadi siku hususan katika nchi maskini duniani. Kuna zaidi ya watoto millioni moja, wengi wao wakiwa ni watoto wa kike wanaonyonywa na kudhulumiwa; wanaonyanyaswa na kutengwa. Baba Mtakatifu Francisko anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuibua mikakati itakayodhibiti kikamilifu janga hili duniani. Watoto wote wanapaswa kuwa na haki ya kucheza, kusoma, kusali na kukua katika familia zao, katika mazingira rafiki, yenye upendo, amani na utulivu. Hii ni haki ya watoto na wajibu wa watu wazima.

Watoto wanaoishi katika mazingira yenye utulivu yanawawezesha watoto kuwa na matumaini ya maisha bora kwa siku za usoni. Ole wao wanaozima cheche za furaha ya matumaini miongoni mwa watoto!







All the contents on this site are copyrighted ©.