2013-06-12 07:35:48

Kongamano la Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani!


Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 17 Juni 2013 litakuwa na Kongamano la Utoto Mtakatifu, linalofanyika Jimboni Ifakara na linaloongozwa na kauli mbiu "Mtoto ni Imani". Kongamano hili linafanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita. RealAudioMP3

Wanachama wa Utoto Mtakatifu kutoka katika Majimbo yanayounda Jimbo kuu la Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine watachambua kuhusu"Mtoto na Mwaka wa Imani; Malezi ya Mtoto na changamoto za utandawazi. Wazazi na walezi wa Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam, wao watashirikishwa kuhusu umuhimu wa walezi katika maisha ya imani na mfano wa maisha ya Kikristo.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, ikihojiana na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari anapenda kukazia kwamba, malezi ya watoto yanapaswa kupata chimbuko lake katika familia. Wazazi wawasaidie watoto wao kufahamu tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu na kijamii, wakitambua kwamba, wao ndio makatekista na walimu wa kwanza kwa maisha ya watoto wao.

Askofu mkuu Rugambwa anaendelea kusema kuwa utume wa Utoto Mtakatifu unaopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania hauna budi kwenda sanjari na dhamana na wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na makuzi ya watoto: kiimani, kimaadili na kiutu. Wazazi na walezi wawashirikishe watoto wao katika maisha na utume wa Kanisa. Watambue na kuthamini maisha ya familia inayoanza pale nyumbani, inakua na kupanuka katika Kigango, Parokia, Jimbo na Kanisa lote katika ujumla wake.

Watoto wafahamishwe umuhimu wa familia na dhamana yake, ili wawe tayari kwa siku za usoni kuisimamia, kuilinda na kuitetea. Wazazi waendelee kushirikiana na Kanisa katika malezi na makuzi ya watoto na kwamba, Utoto Mtakatifu upate chimbuko lake katika Familia na kuendelea kupanuka ili kujenga na kuimarisha Familia ya Mungu inayowajibika katika Kanisa mahalia na katika Kanisa la kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.