Kanisa ni mahali pa kuonja upendo, huruma na matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu!
Baba Mtakatifu Francisko katika mwendelezo wa Katekesi kuhusu Kanuni ya Imani kama
sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jumatano tarehe 12 Juni 2013 kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameendelea kupembua kuhusu Kanisa
kama Familia ya Mungu inayoitwa kuishi maisha mapya katika Kristo. Waamini wanashirikishwa
katika Familia hii kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanamozaliwa kwa Maji na Roho
Mtakatifu, changamoto ya kumwilisha amri ya upendo kwa Mungu na jirani.
Baba
Mtakatifu anawakumbusha Wakristo kwamba, wanayo dhamana inayowataka kuwa ni chachu
ya matumaini ya upendo ulimwenguni ambako watu wamejeruhiwa kwa dhambi na uovu. Licha
ya giza linalowazunguka wanadamu katika maisha haya, lakini waamini wanaalikwa kwa
namna ya pekee kuwa ni mwanga unaoonesha matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Baba
Mtakatifu anasema, wema wa Mwenyezi Mungu una nguvu kubwa zaidi kuliko maovu yanayojionesha
ulimwenguni. Hatima ya maisha ya mwamini ni Ufalme wa Mungu ulioanzishwa hapa duniani
na Yesu Kristo, utakaofikia utimilifu wake kwa kushiriki furaha ya uzima wa milele
mbinguni. Hii ndiyo maana ya Kanisa kuwa ni Familia ya Mungu, kielelezo makini cha
mpango wa upendo wa Mungu kwa Familia ya binadamu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu
anaomba ili Kanisa daima liwe ni mahali ambapo kila mtu anaweza kuonja huruma ya Mungu,
kwa: kukaribishwa, kupendwa, kusamehewa pamoja na kuhamasishwa kuishi vyema mintarafu
misingi ya Injili.
Akizungumza na waamini pamoja na mahujaji kwa lugha mbali
mbali, Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa ni vyombo vya upendo na huruma ya Mungu
kwa watu wake; waendelee kumpenda Kristo na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda makini
wa maisha ya Kiinjili. Waamini wajenge ndani mwao ujasiri na uthabiti wa imani.