2013-06-11 07:58:47

Siku ya vijana inapania pia kukuza na kuimarisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yatakaoanza kutimua vumbi mjini Rio de Janeiro, Brazil kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013, itakuwa ni fursa makini kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kukutana na kusherehekea zawadi ya imani ndani ya Kanisa na changamoto kutoka kwa Kristo mwenyewe anayewahamasisha vijana kutoka kifua mbele kwenda hadi miisho ya dunia ili kuwafanya watu kuwa ni wafuasi wake. RealAudioMP3

Shirika la Wafranciskani katika mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho haya, limeandika barua ya wazi kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakaoshiriki, kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema fursa hii kukuza na kuimarisha wito wao wa Kikristo.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni mwaliko wa kuona na kushuhudia karama mbali mbali ambazo Roho Mtakatifu amelikirimia Kanisa. Kwa mfano wa Watakatifu Clara na Francisko wa Assisi, vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameguswa kiasi kwamba, wameamua kufuata mifano ya imani na maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Familia ya Wafranciskani inasema, inapenda kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kama ifuatavyo: Kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 20 Julai 2013 katika Mji wa Sao Joao dei Rei, kutafanyika mkutano wa kimataifa wa Vijana wa Kifranciskani. Wakati wote wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana, Wafranciskani hawa watakuwa na kibanda cha maonesho ya miito.

Hapa ni mahali pa majadiliano, sala na tafakari bila kusahau kwamba vijana wengi wanapenda muziki, kumbe, patakuwa na burudani ya kukata na shoka. Vijana watapata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa Mashirika ya Kifranciskani. Vijana wote wanaotaka kukumbatia Msalaba wa Kristo na kuupeleka hadi miisho ya dunia wanakaribishwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.