Nia za jumla za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Juni ni kujenga utamaduni wa waamini kuheshimiana,
jambo ambalo linapata chimbuko lake katika majadiliano na hali ya kusikilizana kwa
dhati ili kudumisha heshima. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia ya habari, kumsikiliza jirani yako kwa heshima na taadhima inaweza kuonekana
kuwa ni unyonge.
Lakini, hii ndiyo heshima ambayo inafumbatwa katika kitendo
hiki cha unyenyekevu hasa ikiwa ni mtu ambaye mnasigana kwa mambo mengi. Majadiliano
ni njia muafaka inayoweza kusaidia kukomesha kinzani na migogoro inayoendelea kuibuka
siku hadi siku katika Jamii nyingi.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita anabainisha kwamba, katika ulimwengu huu ambamo kuna mwingiliano mkubwa wa
watu kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuheshimiana; hamu ya kutaka kufahamiana na
kuendeleza majadiliano katika hali ya ukweli, unyenyekevu na upendo. Watu watambue
kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu ni wadhambi na wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi
Mungu. Ni watu wanaohitaji huruma, upatanisho pamoja na kusafisha kumbu kumbu zao
katika ngazi ya mtu binafsi na Jumuiya katika ujumla wake.
Hii ndiyo changamoto
kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka
wake wa Kichungaji mara baada ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, kwani
waamini wanachangamotishwa kuwa mashahidi, wanyenyekevu na wenye moyo wa kusamehe,
mambo yanayojionesha kwa namna ya pekee kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Itakumbukwa
kwamba, Mwezi Juni, Kanisa linafanya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Majadiliano
ya kina ni kielelezo cha upendo na mwaliko wa kuuendelea kushirikiana na wengine kwa
ajili ya mafao ya wengi.
Majadiliano ya kidini yana umuhimu wa pekee katika
ulimwengu wa utandawazi na athari zake, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki,
amani na mshikamano wa kimataifa. Majadiliano ya kidini ni dhamana na wajibu wa Wakristo
na Waamini wa dini nyingine duniani. Kwa Mwezi Juni, Kanisa linaendelea kusali ili
kwamba, liweze kusaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano.
Nia
za Kimissionari za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Juni ni Uinjilishaji Mpya, ili pale ambapo
watu wamemezwa mno na malimwengu, Jumuiya za Kikristo ziwe ni kikolezo cha Uinjilishaji
Mpya. Mwanzoni, nchi nyingi za Ulaya na Marekani zilikuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji
wa watu, lakini katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo wanachangamotishwa
kwanza kabisa kuwa ni Wamissionari katika nchi na familia zao.
Waamini waliomezwa
na malimwengu watambue na kuonja tena umuhimu wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Kuna wimbi kubwa la Waamini wanaotoka Kanisani kwa kuona kwamba, kweli na mafundisho
ya kiimani hayana tena nafasi katika maisha yao, kiasi cha kudhani kwamba, Mungu hayupo
tena!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto anabainisha kwamba, Uinjilishaji Mpya
unakwenda sanjari na toba na wongofu wa ndani. Njia muafaka ya Uinjilishaji Mpya ni
kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kwa njia hii waamini wataweza kuona
tena ndani mwao ile heshima ya kuwa ni Wana wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano
wake, wakakombolewa kutoka katika dhambi na mauti kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo;
sasa wanafurahia matunda ya imani ambayo wangependa kuwashirikisha pia jirani zao
wale walioko karibu na wale ambao wako mbali.
Waamini wanachangamotishwa na
Mama Kanisa kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji, kwa kutolea ushuhuda makini kwa Injili
ya Kristo na Kanisa lake, hata kwa wale ambao wanaonesha moyo mgumu. Waamini wanaalikwa
kwa namna ya pekee kuwa na ari na mwamko mpya wa maisha ya imani, daima wakijitahidi
kuonesha: imani, furaha na matumaini. Ni mwaliko kutoka kwa Yesu kwamba, waamini wote
wawe ni wavuvi wa watu kwa njia ya ushuhuda amini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa
lake. Uinjilishaji mpya ni njia mpya ya kuzungumza na kutenda katika imani, matumaini
na mapendo.