Mapambano dhidi ya biashara haramu ya watoto duniani!
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Juni inaadhimisha Siku ya Kupambana
na Ajira ya Watoto Duniani. Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco kutoka Hispania limezindua
kampeni ya kupinga biashara haramu ya watoto ambao wanafanyishwa kazi katika mazingira
hatarishi na wakati mwingine kugeuzwa kuwa ni watumwa. Shirika hili kadiri ya taarifa
ya FIDES linasema kwamba, kuna zaidi ya watoto 300,000 kutoka Afrika Magharibi wanaopelekwa
utumwani kila mwaka.
Baadhi yao wanageuzwa kuwa ni watumishi wa nyumbani,
wengine wanapelekwa kufanya kazi katika mashamba makubwa, mashimbo ya madini, kwenye
masoko na kwa wasichana wengi wao wanatumbukizwa kwenye soko la ukahaba. Inasikitisha
kuona kwamba, kuna nchi kadhaa Barani Afrika zimeweka sahihi itifaki ya kimataifa
ya kuwalinda na kuwatetea watoto, lakini bado zinashindwa kuwekeza zaidi katika hatima
hii.
Baadhi ya wazazi na walezi kutokana na umaskini na hali ngumu ya maisha
wamejikuta wanatumbukia katika biashara haramu ya binadamu, hali inayowanyima watoto
hawa fursa ya kusoma na kujiendeleza zaidi. Baadhi ya wazazi wamekuwa wakidanganywa
kwa kupatiwa ahadi ya kuwa na maisha bora zaidi pamoja na kupata fedha, lakini matokeo
yake ni kuambulia patupu!
Umaskini, tamaa ya fedha na utajiri wa haraka haraka;
kinzani na migogoro ya kifamilia; mfumo dume na ukosefu wa usawa miongoni mwa watoto
kwani Jamii nyingi za Kiafrika zinawapendelea na kuwekeza kwa watoto wa kiume kuliko
ilivyo kwa wasichana. Maadhimisho haya yaikumbushe Jamii umuhimu wa kusimama kidete
kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya watu wenye nia mbaya na watoto hawa!