Majadiliano ya kidini yanapania kukuza mema ya kiroho, maadili, tunu msingi za kijamii
na kitamaduni miongoni wa waamini wa dini mbali mbali duniani!
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa
Wakristo kuwa na busara na mapendo kwa njia ya majadiliano na ushirikiano na wafuasi
wa dini mbali mbali; ni mwaliko wa kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha ya Kikristo;
kwa kukuza mema ya kiroho, kimaadili na tunu msingi za kijamii na kitamaduni zinazopatikana
miongoni mwa wafuasi wa dini mbali mbali duniani.
Kwa namna
ya pekee, kuna haja kwa Wakristo na Waislam kuendeleza majadiliano ya kidini kama
sehemu ya mchakato wa kukuza upatanisho, haki na amani, kwa kufanya kazi kwa njia
ya ushirikiano. Hii ni changamoto ya kuondokana na kila aina ya ubaguzi, ukosefu wa
uvumilivu na misimamo mikali ya kiimani ambayo wakati mwingine imekuwa ni chanzo cha
uvunjifu wa amani na utulivu.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika anawasihi
viongozi wa Serikali Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha uhuru
wa kidini: kisheria na kivitendo, ili kila mtu Barani Afrika aweze kuwa na haki ya
kuchagua dini anayotaka bila shuruti; akiwa na haki ya kuabudu pamoja na uhuru wa
dhamiri.
Kwa kutambua changamoto zote hizi, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza,
limeandaa kongamano linalopania kudumisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa waamini
wa dini mbali mbali nchini humo, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 16 Juni 2013. Kardinali
Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anatarajiwa kuhudhuria
na kuwatembelea viongozi wa dini mbali mbali nchini Uingereza. Lengo la mikutano hii
ni kutoa fursa kwa viongozi hawa kuangalia kwa pamoja uwezekano wa kukuza na kuendeleza
majadiliano ya kidini, daima wakitafuta mafao ya wengi, haki na amani.
Hii
itakuwa ni nafasi kwa viongozi wa kidini nchini Uingereza kusali kwa pamoja hapo tarehe
13 Juni 2013 majira ya jioni kwenye Ukumbi wa Kanisa kuu la Westminster. Wawakilishi
wa viongozi wa kidini watatoa sala na maombi yao kwa ajili ya amani kadiri ya mapokeo
yao, kama kielelezo cha ushuhuda wa utashi wa amani duniani. Ni sala inayopania kuendeleza
mshikamano na udugu ulioanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ukaendelezwa
na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa kutambua kwamba, majadiliano ya kidini
ni jambo msingi kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Uingereza linasema kwamba, ziara hii ya kichungaji itakayofanywa na Kardinali Jean
Louis Tauran itakuwa ni fursa nyingine ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini
pamoja na kuimarisha uhusiano uliopo baina ya wafuasi wa dini mbali mbali nchini Uingereza
pamoja na kukuza urafiki miongoni mwao!