Jitokezeni kimasomaso kutangaza Injili ya Kristo bila ya kujibakiza! Mmepewa bure,
toeni bure!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 11 Juni 2013 ameadhimisha Siku kuu ya Mtume
Barnaba aliyejitosa kimasomaso kuhubiri Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia
kwa njia ya maneno lakini hasa zaidi kwa matendo yake. Ibada ya Misa takatifu imefanyika
kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican.
Hii ndiyo
chemchemi ya furaha waliyokuwa nayo waamini wa Kanisa la Mwanzo, kiasi kwamba, waliweza
kuchangia kwa hali na mali kufanikisha jitihada za Uinjilishaji, kwa kutambua kwamba,
yote waliyokuwa nayo wamepata bure na kwa njia hii wanapaswa kuyatumia kwa ajili ya
ustawi na mafao ya Kanisa kwa ujumla.
Baba Mtakatifu anasema, wafuasi wa Kristo
wanaojitosa kikweli kweli kutangaza Injili ya Kristo hawana budi kuchuchumilia fadhila
ya ufukara; kwa kuutolea ushuhuda wa uwepo wa Mungu anayewawezesha katika yote. Kanisa
linapaswa kuonesha ile taswira ya ufukara kwa kutumia vyema rasilimali yake kwa ajili
ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.
Kanisa lijiepushe anasema Baba Mtakatifu
kuwekeza katika mambo ya kidunia kama wafanyavyo wafanyabiashara wanaotafuta mali
na faida kubwa! Vitegauchumi vya Kanisa viwe ni kwa ajili ya huduma na maendeleo kwa
binadamu.
Hiki ndicho kielelezo cha maisha kilichotolewa na Mitume na Wafuasi
wa Yesu; kwa njia ya ufukara wao, wakawa tayari kujitosa kutangaza matendo makuu ya
Mungu. Bila majitoleo ya wafuasi wa Kristo, Kanisa litadumaa na kusinyaa! Changamoto
kwa waamini kujitoa kwa ajili ya Kanisa, kwani wamepewa yote bure na kwamba, wao ni
zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.