2013-06-11 10:09:59

Bado kuna vikwazo vinavyokwamisha mamillioni ya watu duniani kupata huduma bora ya dawa!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni wakati akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu upatikanaji wa dawa alisema kwamba, Vatican inaunga mkono mambo msingi yaliyoainishwa kwenye taarifa iliyotolewa.

Anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu na wa kisheria utakaobaini madhara ya kijamii na kisiasa yanayosababisha mamillioni ya watu kukosa huduma ya dawa ambayo ingesaidia maboresho ya afya ya watu wengi duniani kutokana na vikwazo mbali mbali vilivyopo kwa sasa. Azimio la Umoja wa Mataifa linabainisha kwamba, kila mtu anayo haki ya kupata huduma bora ya afya kwa ajili yake binafsi na familia yake.

Huduma hii ni pamoja na: chakula bora, malazi safi, nguo, huduma za afya na za kijamii pamoja na kuhakikishiwa usalama wake wakati wa ukosefu wa fursa za ajira, ugonjwa, ulemavu, hali ya ujane, uzee na mambo mbali mbali ambayo yako nje ya uwezo wa mwanadamu.

Askofu mkuu Silvano Tomasi anasikitika kusema kwamba, taarifa hii ina mapungufu kidogo kwani hakuna msisitizo wa nguvu uliowekwa katika mchakato wa kukidhi mahitaji muhimu ya mtu binafsi na familia, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu. Watu wengi wanashindwa kupata huduma msingi za afya kutokana na vikwazo vya kisheria, changamoto ya kuweka sheria za haki zinazoongozwa pia na mshikamano wa kimataifa miongoni mwa watu.

Ujumbe wa Vatican katika mada hii unapenda kukazia kwa namna ya pekee kuhusu mamillioni ya watu ambayo yanakosa huduma msingi za afya, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuangalia uwezekano wa kuanzisha haki shirikishi inayomhakikishia kila mtu huduma msingi kadiri ya mahitaji yake. Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapotekeleza wajibu wao katika utoaji wa huduma, kuna haja pia ya kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika mchakato wa kuzuia na kutibu magonjwa ili nao waweze kufaidika na haki zinazotolewa katika sekta ya afya.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anabainisha kwamba, Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa wa utoaji huduma katika sekta ya afya, tangu vijijini hadi kwenye miji mikubwa duniani. Ni huduma inayotolewa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; mahali ambapo hata wakati mwingine, Serikali zinashindwa kutoa huduma kutokana na sababu mbali mbali. Shirika la Afya Duniani linabainisha kwamba, kati ya asilimia 30 hadi 70 ya miundombinu ya sekta ya afya Barani Afrika inamilikiwa na kuendeshwa na Mashirika ya kidini.

Askofu mkuu Tomasi anakiri kwamba, huduma ya sekta ya afya ni nyeti inahitaji kushughulikiwa kwa umakini mkubwa pamoja na kutambua mchango unaotolewa na wadau mbali mbali katika sekta ya afya badala ya kujikita zaidi katika masuala ya sheria, uchumi na siasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.