Mshikamano kati ya
Vatican na Serikali ya Italia kwa ajili ya majadiliano ya kidini na mafao ya wengi!
Uhusiano wa dhati kati ya Vatican
na Serikali ya Italia ni jambo msingi ambalo limemwilishwa katika taasisi na kuota
mizizi yake katika historia sanjari na kukuzwa katika majadiliano ya kidini. Sehemu
ya hotuba iliyotolewa na Rais Giorgio Napolitano wa Italia alipokutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kama kielelezo cha mshikamano kati ya Serikali
na Wananchi wa Italia kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Rais Napolitano anasema kwamba, wakati
Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anaanza utume wake kama Kahlifa wa Mtakatifu Petro,
alikuwepo kushuhudia tukio hili la kihistoria, hapo tarehe 19 Machi 2013, kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na baadaye wakaweza kubadilishana mawazo kidogo kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Rais Napolitano amempongeza Baba Mtakatifu
kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi ambalo lina mvuto na mguso mkubwa
katika maisha na shughuli za kichungaji, hali inayojionesha kwa sasa kutokana na ushiriki
mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Italia, wanaomiminika
kuhudhuria katekesi yake kila jumatano, Sala ya Malaika wa Bwana kila Jumapili na
katika Ibada mbali mbali ambazo amekuwa akiziendesha kama Askofu wa Roma.
Rais
Napolitano anatambua na kukiri jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano
dhidi ya umaskini miongoni mwa watu wake; jitihada za kulinda na kudumisha misingi
ya haki na amani; kutetea zawadi ya maisha na hali tete kwa familia na wakimbizi,
wanaodhulumiwa kutokana na ubinafsi na kwamba, Kanisa na Jamii kwa ujumla inachangamotishwa
kuwahudumia kwa ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati.
Waitaliani ambao kwa miaka mingi walijihesabu
kuwa ni sehemu ya “nchi matajiri”, lakini leo hii kuna mamillioni ya wananchi wanakabiliana
na umaskini na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa
ambao umeonesha makucha yake kwa takribani kipindi cha miaka kumi sasa. Kuna idadi
kubwa ya watu hasa vijana wasiokuwa na fursa za ajira, jambo linalohitaji anasema
Rais Napolitano kufanya tafakari ya kina, kuwa na mwono mpya; kujenga misingi ya haki
na mshikamano na kuwasaidia waathirika wa myumbo wa uchumi kimataifa.
Ni
changamoto ya kuwa na mwelekeo mpya wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii Barani Ulaya,
kwa kutambua na kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza kwa nyakati hizi, bila kusahau
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na nchi changa duniani katika kujikwamua na hali
duni ya uchumi. Lakini mabo yote haya hayana budi kuzingatia misingi ya maisha ya
kiroho na kimaadili, bila kupoteza dira na matumaini.
Rais Napolitano amelipongeza Kanisa kwa
mchango wake wa hali na mali katika maendeleo na ustawi wa wananchi wa Italia, wanapotekeleza
utume na dhamana yao katika shughuli mbali mbali za kichungaji. Serikali ya Italia
itaendelea kushirikiana kwa hali na mali na Vatican kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya watu, haki na amani sanjari na kusimama kidete kutetea uhuru wa kuabudu; majadiliano
ya kidini na kiekumene kwa ajili ya mafao ya wengi.
Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemshukuru
na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa mchango wake makini
katika maisha na ustawi wa Kanisa kwa ujumla.