2013-06-10 08:28:11

Matunda ya upendo na huruma ya Mungu ni maisha mapya!


Mwezi Juni umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu; kisima kinachobubujisha wokovu kwa binadamu wote. Moyo wa Yesu ni kitulizo cha watu waliochoka na kuelemewa na mizigo. Ni Moyo ambao ulitobolewa na humo ikatoka maji na damu, kielelezo cha Sakramenti za Kanisa na utimilifu wa Maandiko Matakatifu kuhusu Mwanakondoo wa Mungu aliyekufa Msalabani na hivyo akawa ni chanzo cha msamaha na maisha mapya.


Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 9 Juni 2013, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, huruma ya Kristo ni nguvu inayomkirimia mwanadamu maisha mapya, kama inavyojionesha kwenye Neno la Mungu, Jumapili ya kumi ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, Yesu alipomfufua kijana wa Naini. Huruma inayooneshwa na Yesu ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu; ndiyo mwelekeo wa Mwenyezi Mungu anapokutana na umaskini, taabu na mahangaiko ya binadamu.


Baba Mtakatifu anasema kwamba, matunda ya upendo na huruma ya Mungu ni maisha mapya, kama ilivyojitokeza kwa yule Mwanamke wa Naini aliyefufuliwa mtoto wake wa pekee, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu anamwangalia na kumsubiri mwanadamu kwa jicho la huruma na upendo mkuu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoogopa kumwendea Kristo, kwani ana Moyo wenye huruma; waamini wakithubutu kumwonesha madonda yao ya ndani, kwa hakika atawaponya na kuwasamehe dhambi zao, kwani Yesu ni kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa Mungu.


Baba Mtakatifu anasema, Moyo Safi wa Bikira Maria umeonja na kushiriki huruma ya Mungu, hasa wakati wa mateso na kifo cha Kristo pale Msalabani. Mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria awasaidie kuwa wapole, wanyenyekevu na watu wenye huruma kwa jirani zao.


Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, aliyaelekeza mawazo yake nchini Poland ambako, Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, amewatangaza Mama Sofia Czeska Maciejowska, Mwanzilishi wa Shirika la Kutolewa Bikira Maria Hekaluni, lililoanzishwa kunako karne ya 17 pamoja na Sr. Margherita Lucia Szewczyk ambaye kunako karne ya 19 alianzisha Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Mateso. Matukio yote haya mawili anasema Baba Mtakatifu yamefanyika kwenye Jimbo kuu la Kracovia, nchini Poland.







All the contents on this site are copyrighted ©.