2013-06-10 09:06:17

Amri 10 za Mungu ni zawadi, kielelezo cha upendo, dira na mwongozo wa maisha adili ili kujenga misingi ya haki, amani, usawa na mapendo!


Katika kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 40 tangu Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu kilipoanzishwa nchini Italia, Jumamosi tarehe 8 Juni 2013, wanachama wake wameshiriki katika tafakari ya kina kuhusu Amri 10 za Mungu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Milano.

Tukio hili limeandaliwa kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye tukio hili amekumbushia umuhimu wa kumwilisha Amri za Mungu kwa kupenda zawadi ya maisha kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Amri 10 za Mungu anasema Baba Mtakatifu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu, hali inayomtuma kuanzisha Agano na binadamu, kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu mwenyewe, changamoto kwa waamini kuonesha imani yao kwa Mwenyezi Mungu. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili katika mchakato wa kujenga na kuimarisha Jamii yenye haki, usawa na mapendo. Jamii inayotamani kushibishwa kwa ukweli, utu na maadili mema. Kuna mmong'onyoko mkubwa wa kimaadili unaotokana na binadamu kumkana na kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake.

Amri 10 za Mungu ni mwongozo makini unaowaelekeza wale wanaotafuta amani, haki, utu na heshima ya binadamu. Hii ni njia ya uhuru wa kweli na sheria ya Mungu ambayo imeandikwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Ni changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kama ilivyokuwa wakati wa Waisraeli pale Mlimani Sinai kuonesha uaminifu kwa Mungu anayewajalia uhuru wa kweli.

Amri za Mungu zinamwonesha mwanadamu uhuru wa kweli kwa kuondokana na utumwa unaowafunga watu wengi katika ubinafsi wao kwa kuwachangamotisha kuishi kwa kuwaheshimu wengine ili kushinda kishawishi cha kupenda mali, madaraka na sifa ucharwa! Watu wajifunze kuwa wakweli na waaminifu; wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira.

Amri 10 za Mungu ni changamoto kwa binadamu kuwa mwaminifu kwake yeye mwenyewe huku akitembea katika heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu. Amri hizi ni sheria ya upendo inayojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho na mwaliko wa kumpenda Mungu na jirani kama unavyojipenda mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Amri hizi zinabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kutoa maana ya maisha yanayomtambulisha mwanadamu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuwa ni kielelezo cha mahusiano yote kati ya Mungu na binadamu. Uhuru wa kweli unajionesha katika kupenda na kuchagua jema katika kila hali na mazingira.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kutambua, kukubali na kumwilisha Amri za Mungu katika maisha yao ya kila siku kwani ni njia ya upendo iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe kwa ajili ya kumlinda mwanadamu na kumwongoza katika ukweli.









All the contents on this site are copyrighted ©.