Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji
Mpya anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, hapo tarehe 15 hadi tarehe 16
Juni 2013 yatakuwa na sura ya pekee, pale ambapo waamini kutoka pande mbali mbali
za dunia watakapokusanyika kusali, kutafakari na kushuhudia pamoja na Baba Mtakatifu
Francisko umuhimu wa zawadi ya maisha ambayo mwanadamu amekabidhiwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Hii ni zawadi
ambayo inapaswa kulindwa na kuheshimiwa, tangu pale mtoto anapokuwa tumboni mwa mama
yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu. Ni zawadi
ya maisha inayojionesha miongoni mwa wazee na wagonjwa walioko kufani, wanaonyemelewa
na utamaduni wa kifo kutokana na baadhi ya watu wachache ndani ya Jamii kutaka kukumbatia
sera za kifo laini na utaoaji mimba, mambo ya kutisha lakini baadhi ya watu wanaanza
kuyaona kuwa ni ya kawaida.
Askofu mkuu Fisichella anasema kwamba, hii itakuwa
ni fursa maalum ya kuendelea kuwatia shime, wale wote wanaosimama kidete kulinda na
kutetea zawadi ya maisha, huku wakijitahidi kufuata nyayo za Kristo mchungaji mwema,
kwa kuwamegea watu utajiri unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo, kwani Kristo
mwenyewe anasema, “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele”. Hiki ndicho
kiini cha Ujumbe uliomo kwenye Waraka wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Evangelium
Vitae, Injili ya Uhai.
Askofu mkuu Fischella anasema, watu wengi wameonesha
nia ya kushiriki katika tukio hili la kihistoria wakati huu Mama Kanisa anapoendelea
kuadhimisha Mwaka wa Imani, ili umati wa waamini na watu wenye mapenzi mema utakaokuwa
umekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uweze kupiga kelele ya
kutetea Injili ya Uhai hadi miisho ya dunia.
Kwa siku mbili, Baraza la Kipapa
la Uhamasishaji wa Uinjili Mpya litaendesha semina elekezi kuhusu yaliyomo kwenye
Waraka wa Kichungaji wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, Injili ya Uhai. Mama Kanisa
anapenda kuhakikisha kwamba, Injili ya Uhai inaendelea kupewa kipaumbele cha pekee
katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Tarehe 15 Juni 2013, Warsha kwa ajili
ya wazungumzaji wa Lugha ya Kiingereza itafunguliwa kwenye Chuo Kikuu cha Urbaniana.
Kardinali Raymond Leo Burke atatoa hotuba elekezi. Askofu mkuu Joseph Augustine di
Noa ataongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwenye Kanisa la Santo Spirito in
Sassia, lililoko karibu na Vatican na baadaye yatafuatia Maandamano ya waamini wakiwa
wamebeba mishumaa kuelekea kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya sala na
kesha.