Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anasema, Maadhimisho ya Mafumbo
ya Imani yawasaidie waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwani huu ndio wito
wa kwanza kabisa kwa kila mwamini. Wanaalikwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni
alivyo mtakatifu.
Utakatifu
ni dhamana ya kila Mkristo mbatizwa ambayo kwa njia ya Mlango wa Imani, ameondolewa
dhambi ya asili na hivyo kupatiwa neema ya utakaso inayomwezesha mwamini kuliendea
Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya utakatifu wote.
Askofu mkuu Paul Ruzoka
anasema kwamba, Mapadre wamepewa dhamana ya kuwaongoza waamini katika hija ya utakatifu
wa maisha. Lakini, anawakumbusha Makleri kutambua kwamba, wao wamepewa neema hii kwanza
kabisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na baadaye katika Sakramenti ya Daraja Takatifu.
Hivyo, kuna umuhimu wa pekee kabisa kwa Makleri kuchuchumilia utakatifu wa maisha
unaojionesha katika maisha na utume wao.
Utakatifu wa maisha ni changamoto
inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Makleri wawaonjeshe
waamini na watu wenye mapenzi mema, harufu ya utakatifu na kwamba, waamini wajitahidi
kumwilisha imani kwa njia ya matendo adili, kielelezo cha utakatifu wa maisha.