Wanaotaka kubinafsisha gesi asilia Mtwara wamtibua tena Kikwete!
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesisitiza kuwa pamoja na kweli kwamba gesi
asilia imegundulika mkoani Mtwara lakini gesi hiyo siyo mali ya Wana-Mtwara bali ni
raslimali ya Watanzania wote ambao wataitumia kwa manufaa ya nchi nzima. Hata hivyo,
Rais Kikwete amesema kuwa wananchi wa Mtwara wanayo haki ya kunufaika na gesi hiyo
asilia kama walivyo Watanzania wengine katika sehemu zote za nchi.
Rais
Kikwete ameyasema hayo Jumapili Juni 2, 2013, wakati alipokutana na kuzungumza na
Jumuiya ya Watanzania wanaoishi katika Japan kwenye Hoteli ya Royal Park Yokohama
mjini Yokohama. Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya wiki moja nchini Japan ambako
alihudhuria Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika – TICAD
V (Tokyo International Conference on African Development).
Akizungumza na Watanzania
hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa raslimali yoyote inayogundulika katika sehemu yoyote
ya Tanzania ni mali ya Watanzania wote na lazima itumike kuwanufaisha wote na siyo
wale ambako raslimali hiyo imepatikana.
Katika risala yao, Watanzania walikuwa
wameeleza kutofurahishwa kwao na ghasia na fujo ambazo zimekuwa zinafanywa Mtwara
na baadhi ya watu wanaojiita wakazi wa Mkoa huo wakidai kuwa gesi asilia hiyo ni lazima
itumike kuwanufaisha wananchi na Mtwara badala ya kuisafirisha kwenda Dar Es Salaam
kuzalisha umeme kwa ajili ya nchi nzima.
Rais amesisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika
kuwa raslimali ya nchi inaweza kuzuiliwa isitoke katika eneo ambako inapatikana kwa
vile hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu jambo la namna hiyo. “Hiyo nchi haipo
duniani na wala sera za namna hiyo haziwezi kuanzia Mtwara. Sijui hii dhana wamepata
wapi. Nadhani wanavurugwa na wanasiasa ambao wanajitafutia umaarufu. Mafuta ya Texas
pale Marekani ni ya Wamarekani wote siyo ya watu wa Texas. Mafuta ya North Sea pale
Uingereza ni ya Uingereza yote,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Pato letu
la taifa linachangiwa na kila raslimali yetu – migebuka ya Kigoma inachangia, sato
wa Mwanza wanachangia, almasi ya Mwadui, dhahabu, pamba na kahawa vyote kwa pamoja
vinachangia pato letu la taifa ambalo tunaligawana kwa maendeleo ya kila mmoja wetu.
Kule Mtwara kuna mengi yamefanyika kwa nini mbona wana-Mtwara hawajiulizi pesa ya
kuyafanya hayo ilitoka wapi? Mbona hawadai kuwa hata korosho isitoke Mtwara?”
Rais
Kikwete amekumbusha kuwa siyo mafuta yote yatakayosafirishwa nje ya Mtwara. “Kama
nilivyosema ni asilimia 14 tu ya mafuta ambayo itasafirishwa nje ya Mtwara. Asilimia
kubwa itabakia Mtwara. Kuna viwanda vingi kiasi cha 47 vitajengwa Mtwara vingi kuliko
vilivyo katika eneo lolote la nchi yetu. Linalosubiriwa ni kukamilika kwa upimaji
mkubwa wa Mji wa Mtwara na maeneo ya jirani.”
Amesema kuwa ni jambo la kushangaza
kuwa wana-Mtwara wanadai kuwa gesi asilia isitoke Mtwara. “Sasa gesi isipokwenda sokoni
wana-Mtwara watanufaika vipi? Gesi asilia hii ni lazima iuzwe ili fedha ziweze kupatikana
na kuwanufaisha wana-Mtwara na Watanzania wengine.” Rais Kikwete amesema ni jambo
la kushangaza vile vile kuwa watu wanaandamana leo kuhusiana na mapato ya gesi. “Mapato
ya gesi hii hayataanza kuonekana kati ya miaka sita hadi 10 kuanzia sasa, sasa tunatoana
macho ya nini wakati uwekezaji ndio kwanza umeanza?”
Rais Kikwete ambaye aliandamana
na mawaziri kwenye mkutano huo na Watanzania aliwataka mawaziri hao mmoja mmoja
kuelezea maswali na maoni ya Watanzania hao kuhusu maeneo yao. Mawaziri hao ni
Waziri wa Uchukuzi Dr. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo na Waziri wa Kazi na Ajira Gaudensia Kabaka.