Mapato na matumizi ya wizara ya fedha Tanzania kwa mwaka 2013/14
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge
lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2013/14.
2. Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya
Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa
(Mbunge wa Mufindi Kaskazini) na Makamu wake Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mbunge
wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua
mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mheshimiwa Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Mashariki)
pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao makini. Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara
imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja
mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2012/13.
3.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa
Saada Mkuya Salum (Mb) na Mheshimiwa Janeth Zebedayo Mbene (Mb). Aidha, napenda kutoa
shukrani za dhati kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wakiongozwa
na Katibu Mkuu, Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu Dkt. Servacius B.
Likwelile, Ndugu Elizabeth J. Nyambibo pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ndugu
Laston T. Msongole kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kusimamia utekelezaji wa majukumu
ya Wizara. Vile vile, napenda kuwashukuru Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dkt.
Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Wakuu wa Taasisi
na Wakala wa Serikali, chini ya Wizara kwa michango yao katika kuboresha utekelezaji
wa majukumu ya Wizara.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA
KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13 NA MALENGO YA MWAKA 2013/14
4. Mheshimiwa
Spika, uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa Mpango na Bajeti ya Wizara unazingatia
mambo yafuatayo: Malengo ya maendeleo ya Milenia 2015; Dira ya Taifa ya Maendeleo
ya mwaka 2025; Awamu ya pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania
(MKUKUTA II); Vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano wa mwaka 2011/12 - 2015/16; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010; Mkakati
wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Mwongozo wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2013/14-2015/16;
pamoja na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma - Public Finance Management
Reform Programme (PFMRP).
Usimamizi wa Uchumi 5. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Pato la Taifa liliendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa
asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011, ikiwa ni zaidi ya lengo la
asilimia 6.8 mwaka 2012. Sekta ya fedha ambayo inasimamiwa na Wizara ya Fedha ilichangia
kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Katika mwaka 2012,
sekta hii ya Fedha ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia
1.7 mwaka 2011. Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na utekelezaji madhubuti wa Programu
ya Maboresho ya Sekta ya Fedha. 6. Mheshimiwa Spika, katika kipindi
hicho cha mapitio, Wizara pia ilitekeleza Sera ya Fedha na bajeti kwa lengo la kupunguza
ukwasi na mfumuko wa bei ambapo Benki Kuu ya Tanzania iliongeza mauzo ya fedha za
kigeni katika soko la fedha kama njia mojawapo ya kudhibiti mfumuko huo. Aidha, Benki
ilipandisha kiwango cha chini cha akiba ya amana za Serikali katika mabenki kutoka
asilimia 30 hadi asilimia 40 pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni
kulingana na mitaji yao kwa mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba
2012. Hatua zote zilisaidia kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia
18.7 mwezi Aprili 2012 hadi asilimia 9.4 mwezi Aprili 2013 pamoja na kusaidia kuimarika
kwa kiwango cha ubadilishaji wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani. Aidha, katika
kuimarisha usimamizi na maendeleo ya sekta ya fedha, Wizara imerekebisha muundo wake
kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha – Financial Sector Development
Division ambayo itasimamia uandaaji na utekelezaji wa sera za sekta ya fedha na taasisi
ndogo za fedha kama SACCOS na VICCOBA.
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji
wa Bajeti ya Serikali
7. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kusimamia
uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya matumizi ya kawaida na miradi ya
maendeleo. Wizara imeratibu maboresho ya uandaaji wa bajeti ya 2013/14 kwa kuzingatia
mzunguko mpya wa bajeti. Aidha, Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14,
uliandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kusambazwa kwa wakati. Vile vile,
Wizara imeandaa na kusambaza nyaraka muhimu za bajeti ikiwa ni pamoja na vitabu vya
bajeti ya Serikali (volume I, II, III na IV) kama vilivyopitishwa na Bunge na kitabu
kinachotoa maelezo ya Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati kwa mwaka
2012/13 - 2014/15. Kitabu hiki kinasaidia kuwajulisha wananchi na wadau wengine kuhusu
matokeo ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita pamoja na mwelekeo wa bajeti ijayo
kwa kipindi cha muda wa kati. Kadhalika, katika kuboresha uelewa wa bajeti ya Serikali
kwa wananchi, Kitabu cha Bajeti Toleo la Wananchi kwa mwaka 2012/13 kimeandaliwa na
kusambazwa kwa wakati na kuwekwa kwenye tovuti ya Wizara. Kitabu hiki kimesaidia kueleza
bajeti kwa wananchi wa kawaida kwa lugha rahisi na hivyo kuongeza uwazi katika kutoa
taarifa muhimu za kibajeti.
8. Mheshimiwa Spika, katika kujenga
uwezo wa kuandaa mipango na bajeti kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Wizara ilitekeleza yafuatayo: kufanya tathmini ya mchakato wa
bajeti ya 2012/13 kuhusu namna bajeti ilivyoandaliwa, changamoto zilizojitokeza na
jinsi ya kuzitatua; kuwajengea uwezo maofisa wa bajeti wa Wizara, Idara, Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu kuandaa bajeti ya 2013/14, maboresho
yaliyofanywa kwenye Mfumo wa Kugawa Fedha za Bajeti - Strategic Budget Allocation
System (SBAS) na kuandaa bajeti inayozingatia utendaji -Performance Based Budgeting;
na kuhuisha Mwongozo wa kuandaa mipango na bajeti, ambao umezingatia mzunguko mpya
wa bajeti. Wizara imeendelea kusimamia malipo ya mishahara ya kila mwezi kwa ajili
ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa.
Usimamizi wa Misaada na Mikopo 9. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ili kupata matokeo
yaliyotarajiwa. Mafunzo ya mfumo wa kutunza takwimu na kumbukumbu zingine za misaada
na mikopo yalitolewa kwa Maafisa kutoka Wizara 21 na Washirika wa Maendeleo wapatao
20. Aidha, mapitio ya utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA),
2006 – 2011 wenye lengo la kuimarisha usimamizi wa misaada, yalifanyika.
10.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha usimamizi wa misaada na mikopo ya kibajeti, Wizara
iliandaa mkutano wa Mwaka wa Mapitio ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti - General Budget
Support Annual Review meeting uliofanyika mwezi Novemba 2012. Matokeo yaliyotokana
na Mkutano huo ni washirika wa Maendeleo kuipatia Serikali misaada ya kibajeti yenye
thamani ya sh. bilioni 1,163.13 fedha ambayo imepangwa kutumika katika bajeti ya 2013/14.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeimarisha Mfumo wa Mapitio
ya Matumizi ya Umma - Public Expenditure Review (PER) kwa kuanzisha Sekretarieti
ya pamoja yenye wajumbe wa upande wa Serikali na upande wa Washirika wa Maendeleo
pamoja na kuandaa Mpango Kazi wa mwaka.
11. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/14, Wizara inatarajia kukamilisha Mfumo mpya wa Ushirikiano wa Kimaendeleo
-Development Cooperation Framework , kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mfumo
huu ndio utakaoongoza usimamizi wa Misaada na Mikopo ya Kibajeti katika kutekeleza
mipango na programu za kitaifa za kukuza uchumi, kupunguza umaskini na kuleta maendeleo.
Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya Mfumo wa Kutunza Kumbukumbu za Misaada na
Mikopo - Aid Management Platform kwa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na Asasi za
Kiraia. Vile vile, Wizara itaendelea kuandaa mikutano ya kila mwaka ya Mapitio ya
Misaada na Mikopo ya Kibajeti pamoja na Mapitio ya Matumizi ya Umma.
Uhimilivu
wa Deni la Taifa 12. Mheshimiwa Spika, serikali inasimamia Deni la Taifa
kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa kusimamia Deni na Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka 2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo,
mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya kuangalia uhimilivu wa Deni la Taifa na viashiria
vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa vinaonesha kuwa, deni
la taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati. Mathalani, uwiano wa thamani
ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt) kwa Pato la Taifa (GDP) ni asilimia
18.9 ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50. Hii ni ishara kuwa kiwango cha kukua
kwa Deni la Taifa ni kidogo ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kiashiria
kingine muhimu ni uwiano wa thamani ya sasa ya Deni la Taifa (Present Value of Debt)
kwa thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi (export) ni asilimia 56.2 ikilinganishwa
na kiwango cha cha ukomo ambacho ni asilimia 200. Hii ni ishara nyingine inayotuhakikishia
kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa kuwa kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa ni ndogo ikilinganishwa
na uwezo wan chi kulipa deni hilo kwa mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa na humuma
nje ya nchi.
13. Mheshimiwa Spika, katika mkakati wa kuboresha
mfumo wa usimamizi wa Deni la Taifa serikali inakamilisha taratibu za kuanzishwa kwa
Idara kamili ndani ya Wizara ya Fedha pamoja na kupitia upya Mkakati wa taifa wa kusimamia
madeni wa mwaka 2002 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada
ya mwaka 1974 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004 na hivyo kuboresha muundo uliopo wa
usimamizi wa Deni la Taifa pamoja na sheria yake.
Usimamizi wa Matumizi ya
Fedha za Umma
14. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2012/13,
Wizara ilitekeleza yafuatayo: kuboresha Mfumo wa Malipo Serikalini – Integrated Financial
Management System(IFIMS) kutoka mfumo wa toleo la EPICOR 7.3.5 kwenda toleo la EPICOR
9.05 kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma; kukamilisha
zoezi la kutoa mafunzo ya kufanya malipo moja kwa moja benki kwa njia ya kielektroniki
-Tanzania Inter-Bank Settlement System (TISS) kwa watumishi wa Hazina ndogo zote,
Bunge, Mikoa, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI na Idara ya Ushirika, ikiwa ni maandalizi
ya kuunganisha Taasisi hizo kwenye mtandao wa TISS ili kuboresha usimamizi wa fedha
za umma.
15. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Wahasibu 200
kutoka mikoa 25 walipata mafunzo juu ya usimamizi wa fedha za umma; Wahasibu 425 kutoka
wizara mbalimbali na Sekretarieti za Mikoa walipata mafunzo juu ya Viwango vya kimataifa
vya kiuhasibu vya kuandaa Hesabu za Serikali – International Public Sector Accounting
Standards (IPSAS) na watumishi 120 kutoka katika Wizara na Taasisi walipata mafunzo
ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic
Planning kwa lengo la kujenga uwezo wa idara za bajeti na Mipango katika kutekeleza
maboresho ya usimamizi wa Fedha za umma.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi
wa Fedha za Umma – Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)
16.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea
kutekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma-PFMRP ambapo Awamu
ya Nne ya Programu ilianza kutekelezwa Julai 2012 na itakamilika Juni 2017. Programu
ya PFMRP pamoja na mambo mengine, imewezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanza kutumia
akaunti sita za benki badala ya akaunti nyingi zilizokuwepo kwa lengo la kuendelea
kuboresha usimamizi wa fedha za Umma. Aidha, Programu ilitoa fedha za kuwezesha Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa Mpango Mkakati wake wa Programu ya Usimamizi wa Fedha
za Umma. Vile vile, matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa programu yaliyofanywa kama
sehemu ya mapitio ya mwaka ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti yaliyofanyika mwezi Novemba
2012 yalionesha kuwa utekelezaji wa Programu ulikuwa wa kuridhisha, na uzingatiaji
wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika kufanya ununuzi ulifikia asilimia 74.
17.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutekeleza Mpango kazi wa miaka mitano wa kuiwezesha
Serikali Kuu kuandaa hesabu kwa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu –International Public
Sector Accounting Standards (PSAS) accrual basis. Kwa mara ya kwanza, hesabu za Wizara,
Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa fedha unaoishia
tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo. Aidha, Wizara imeandaa
miongozo mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea uwezo na uelewa wahasibu
na wadau mbalimbali. Katika kuimarisha usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali
pamoja na utoaji wa taarifa zenye ubora na uwazi, Wizara imeendelea kusimamia na kuimarisha
mtandao wa malipo ya Serikali katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Hazina Ndogo pamoja
na Vikosi vya Jeshi.
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14,
Wizara itaendelea kusimamia, kuimarisha na kudhibiti mapato na matumizi ya fedha za
Serikali kwa kuboresha mtandao wa malipo wa Serikali. Aidha, Wizara itatoa ushauri
wa kitaalamu na kuunganisha Hazina Ndogo na Sekretarieti za Mikoa ili kuziwezesha
kufanya malipo kwa njia ya ki-elektroniki (TISS) kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Vile
vile, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wahasibu wa Wizara,
Mikoa, na Idara za Serikali ya kuandaa hesabu katika viwango vya kimataifa –IPSAS
Accrual basis na kuongeza uelewa wa matumizi ya mtandao wa EPICOR 9.05.
Sera
ya Ununuzi wa Umma
19. Mheshimiwa Spika, katika eneo la Sera ya Ununuzi
wa Umma, Wizara imetekeleza yafuatayo: kukamilisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Ununuzi
wa Umma; kukamilisha rasimu ya Kanuni za Ununuzi wa Umma; kuendelea kuhuisha taarifa
za maofisa Ununuzi na Ugavi katika daftari ambapo jumla ya Maofisa 989 wameingizwa
katika daftari hilo. Aidha, Wizara imeendelea na taratibu za kuanzisha kada ya Ununuzi
Serikalini pamoja na kusimamia na kuendeleza kada ya Ugavi nchini.
20.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara imepanga kufanya yafuatayo:
kuanza utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kufuatilia na kufanya tathmini
ya mfumo wa Ununuzi wa Umma; na kuendelea kuhakiki daftari la taarifa za maafisa Ununuzi
na Ugavi Serikalini.
Mpango wa Millenium Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
21.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia MCA-T imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi
inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia shirika la Millennium Challenge Corporation
(MCC). Utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea vizuri licha ya changamoto ambazo zimeathiri
kasi ya utekelezaji kama vile mvua nyingi kwa mikoa ya Ruvuma na Rukwa na matatizo
ya kiufundi. Ujenzi wa barabara ya Tanga- Horohoro ulikamilika kwa kiwango cha lami
na kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Oktoba 2012; ujenzi wa barabara za ukanda wa Mtwara
yaani Songea – Namtumbo na Peramiho – Mbinga na ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kisiwa
cha Mafia unaendelea. Aidha, kazi ya kuweka lami katika barabara tano za Pemba ya
Vijijini Kaskazini imeanza na ujenzi wa barabara ya Tunduma – Sumbawanga ambao umegawanywa
katika sehemu tatu; Tunduma – Ikana, Ikana – Laela na Laela – Sumbawanga unaendelea.
22. Mheshimiwa Spika, Miradi ya kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini
ya bahari na ule wa ukarabati wa mtandao wa umeme kwa mkoa wa Dodoma imekamilika.
Utekelezaji wa miradi mingine ya ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme, ukarabati
wa mtandao wa umeme kwa mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza na Kigoma,
ikiwa ni pamoja na mradi wa umeme wa Jua Kigoma, inaendelea. Aidha, miradi ya upanuzi
wa mtambo wa maji Ruvu chini na ukarabati wa mfumo wa maji kwa Manispaa ya Morogoro
nayo pia inaendelea.
23. Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji
wa kuridhisha wa miradi, katika kikao cha Bodi ya MCC kilichofanyika mwezi Desemba
2012, kiliamua kuikubalia Tanzania kuidhinisha maandalizi ya Mpango wa Pili wa miradi
ya MCC (MCC Compact II). Serikali imeshaanza maandalizi hayo baada ya kuunda sekretarieti
ya uratibu
Ukaguzi wa Ndani
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
wa fedha 2012/13, Wizara imeandaa na kutoa miongozo ya Usimamizi wa vihatarishi katika
Sekta ya Umma pamoja na Mwongozo wa Uhakiki wa Ubora wa Ukaguzi wa Ndani. Miongozo
hii ilizinduliwa mwezi Machi, 2013. Aidha, Wizara imetayarisha Mwongozo wa Ukaguzi
wa Ndani kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na unategemewa kuanza kutumika rasmi
mwezi Julai, 2013. Kadhalika, Wizara imekamilisha Mkataba wa Makubaliano kati ya Wakaguzi
wa Ndani na Wateja wake na pia kutoa kanuni za maadili ya wakaguzi wa ndani. Miongozo
hiyo ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.
Ukaguzi wa Hesabu
za Serikali
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 Ofisi
ya Taifa ya Ukaguzi iliendelea kutekeleza yafuatayo: kufanya ukaguzi wa hesabu za
mafungu yote ya Wizara na Idara za Serikali, Mikoa ya Tanzania Bara, Halmashauri,
Mashirika ya Umma, Balozi na Wakala wa Serikali; kukamilisha ripoti tano za ukaguzi
wa ufanisi -Value for Money Audit ambapo taarifa zote hizi zimewasilishwa hapa Bungeni
tarehe 11 Aprili 2013; ukaguzi wa Mashirika 50 ulikuwa unaendelea katika hatua mbalimbali
za ukaguzi; Ofisi imeendelea kukiimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ufanisi kwa kutoa
mafunzo kwa watumishi saba na kukipatia vitendea kazi zaidi. Aidha, ofisi iliendelea
kulipia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 53 waliopo katika vyuo mbalimbali na kugharamia
mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 400. Vile vile, ujenzi wa ofisi unaendelea katika
mikoa ya Dodoma na Rukwa na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2014.
26.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/14, Ofisi itatekeleza shughuli zifuatazo:
kuendelea kutekeleza mkakati wa kuwaondoa wakaguzi katika ofisi za wakaguliwa; kufanya
ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini ili kukidhi matakwa
ya sheria ya vyama vya siasa na kuendelea kufanya mazungumzo na Msajili wa vyama vya
siasa namna ya kutekeleza Sheria ya Gharama za Uchaguzi; na kuziimarisha Kamati za
Bunge za Hesabu za Serikali – Public Accounts Committee (PAC) na Local Authorities
Accounts Committee (LAAC), Kamati ya Bajeti na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara
kwa kuzijengea uwezo.
27. Mheshimiwa Spika, shughuli nyingine zitakazotekelezwa
ni pamoja na: kuhakiki matumizi ya fedha za Halmashauri; kushiriki kikamilifu katika
jukumu jipya la kukagua Taasisi za Umoja wa Mataifa ambapo ofisi inaingia mwaka wa
pili wa kuwepo kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa -UN Board of Auditors; kufanya
kaguzi sita za thamani ya fedha; kuendelea na uunganishaji wa ofisi za Ukaguzi zilizoko
mikoani na makao makuu kwa kutumia Mtandao Mpana -Wide Area Network (WAN); kuimarisha
ukaguzi wa kiutambuzi - Forensic audit; na kuongeza idadi ya watumishi.
Sheria
na Miswada ya Fedha
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13,
Wizara iliendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali ili kuweka usimamizi mzuri
wa kodi na fedha za umma. Baadhi ya sheria zilizofanyiwa marekebisho ni sheria mbalimbali
za kodi ambazo zilipitishwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 - The Finance Act,
2012 na Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria
ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali iliyopitishwa na Mkutano wa Bunge wa mwezi Februari,
2013. Aidha, marekebisho ya Mkataba wa Cotonou unaohusu ushirikiano baina ya nchi
za Jumuiya ya Ulaya, Afrika na Visiwa vya Caribbean ambapo Tanzania ni mwanachama,
yalipitishwa na Bunge kupitia Azimio la Bunge katika Mkutano wa mwezi Novemba, 2012.
29.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliandaa kanuni mbalimbali ili kuwezesha usimamizi na
utekelezaji wa Sheria za Kifedha. Baadhi ya kanuni zilizotolewa ni zile za; kuanzisha
credit Reference Databank ya Utunzaji wa Taarifa za Wateja wa Benki na Taasisi za
Kifedha; Pamoja na Credit Reference System. Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki katika
Ukusanyaji wa Kodi ya Mapato; Usimamizi wa Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa abiria wa ndege ambao sio raia wa Tanzania; Kanuni za Sheria ya Udhibiti wa Fedha
Haramu; na Kanuni za Sheria ya Uwekaji Stempu kwenye kazi za Wasanii.
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara itaendelea kukamilisha maandalizi
ya kuwezesha kutungwa kwa Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani – Vale Added
Tax (VAT), Sheria ya Utawala wa Kodi - Tax Administration Act, Sheria ya Hoteli -
Hotels Tax Act, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mfuko
wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - Government Employees Provident Fund (GEPF). Aidha,
Wizara inatarajia kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho kwenye Sheria ya
Usimamizi wa Fedha za Umma, pamoja na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ili kuihuisha
kulingana na mazingira ya sasa ya uchumi. Vile vile, wizara itaandaa kanuni mbalimbali
zitokanazo na sheria hizi ili kuwezesha utekelezaji wake.
Usimamizi wa Mashirika
na Taasisi za Umma
31. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia
utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na Taasisi zake. Majukumu yaliyotekelezwa kwa
kushirikiana na Shirika Hodhi - Consolidated Holding Corporation (CHC) ni pamoja na
kuendelea na zoezi la urekebishaji wa mashirika yaliyo na matatizo katika sekta za
Usafirishaji, Madini, Mawasiliano, Utalii na Fedha.
32. Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepata ofisi katika jengo la CHC Mtaa wa Samora
na tayari watumishi wamehamia katika ofisi hiyo. Katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara
kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia utendaji
wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma na kuboresha utawala bora kwa
kuingia Mikataba ya Utendaji -Performance Contracts na Bodi za Mashirika ya Umma;
kusimamia mikakati ya kurekebisha Mashirika ya Umma na uperembaji wa Mashirika ya
Umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma ili
kuongeza ufanisi na mapato ya Serikali.
Mafao ya Wastaafu na Mirathi
33.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za pensheni, Wizara imeanza utaratibu wa
kulipa Pensheni kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu badala ya vipindi vya miezi sita
sita kuanzia Januari, 2012. Katika utaratibu huu, Wastaafu wanalipwa Pensheni ya miezi
miwili mapema - in advance badala ya miezi mitano iliyokuwa inalipwa katika utaratibu
wa awali. Pensheni inalipwa mwishoni mwa miezi ya Julai, Oktoba, Januari na Aprili.
Aidha, Wizara imeendelea na kazi ya kuweka kumbukumbu za Wastaafu waliopo kwenye daftari
la Pensheni la Hazina kwenye Mfumo wa Kompyuta ujulikanao kwa jina la SAPERION kwa
lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Hadi kufikia mwezi Aprili 2013, kumbukumbu
za Wastaafu 106,030 ziliwekwa kwenye mfumo wa kompyuta. Zoezi hili litaendelea kufanyika
katika mwaka 2013/14 ili kukamilisha uhifadhi wa kumbukumbu za Wastaafu wote wanaolipwa
kupitia Hazina.
34. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia
na kuratibu shughuli za mifuko ya pensheni iliyo chini ya Wizara ya Fedha. Mifuko
hiyo ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika
ya Umma (PPF) na Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF). Mfuko wa Pensheni
kwa Watumishi wa Umma - PSPF
35. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili,
2013 Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma ulisajili wanachama 332,067. Katika
kipindi hicho, Mfuko pia ulikusanya jumla ya shilingi bilioni 446.12. Kati ya makusanyo
hayo, michango ya wanachama ni shilingi bilioni 374.76 na mapato yatokanayo na vitega
uchumi ni shilingi bilioni 71.36. Matarajio ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni
749.10 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2012/13. Aidha, thamani ya Mfuko hadi tarehe
30 Aprili, 2013 ilifikia shilingi bilioni 1,112.24 na unatarajiwa kufikia shilingi
bilioni 1,226.59 mwezi Juni, 2013. Jumla ya shilingi bilioni 422.16 zilitumika kulipa
mafao ikiwa ni pamoja na mafao ya kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi sawa na
asilimia 93.21 ya lengo la mwaka. Vile vile, ili kuongeza wigo wa wanachama, Mfuko
umeanzisha mpango maalum wa kuchangia kwa hiyari kwa watumishi wa sekta rasmi na isiyo
rasmi.
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/14, Mfuko
unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 680.55, kati ya makusanyo hayo, michango
ya wanachama ni shilingi bilioni 539.18, na mapato yatokanayo na vitega uchumi ni
shilingi bilioni 141.37. Aidha, thamani ya Mfuko inatarajiwa kufikia shilingi bilioni
1,522.01. Mfuko unatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 522.32 kwa ajili ya mafao
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiinua mgongo na pensheni za kila mwezi, ambapo jumla
ya wanachama wapatao 7,647 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria. Vile vile, Mfuko
unatarajia kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1,211.39 kwenye maeneo mbalimbali ya
vitega uchumi.
Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini - GEPF
37.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2013 Mfuko umesajili jumla ya wanachama 6,755
wakiwemo wananchi waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi. Katika kipindi hicho
michango ya wanachama ilifikia kiasi cha shilingi bilioni 22.74 sawa na asilimia 64.60
ya malengo ya mwaka mzima. Mapato yatokanayo na vitega uchumi yamefikia shilingi
bilioni 11.64 ambayo ni sawa na asilimia 72.75 ya malengo ya mwaka mzima na thamani
ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 190.0 Machi, 2013. Aidha, Mfuko umelipa
mafao ya shilingi bilioni 7.13 hadi kufikia Machi, 2013 na kufungua ofisi katika Manispaa
za Temeke, Kinondoni na Ilala kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Mfuko utaendelea na jitihada zake
za kuboresha huduma kwa wanachama, kutanua wigo wa wanachama, kukuza mapato yatokanayo
na uwekezaji na kusajili wanachama wengi zaidi kupitia Mpango wa Hiari wa kujiwekea
akiba ya uzeeni na wa lazima. Aidha, Mfuko unatarajia kusajili jumla ya wanachama
16,500 na kukusanya michango yenye thamani ya shilingi bilioni 40.50. Vile vile, mapato
ya vitega uchumi yataongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 19.24 na thamani ya Mfuko
inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 227.
Mfuko wa Pensheni wa Mashirika
ya Umma - PPF
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Mfuko ulikusanya
shilingi bilioni 229.1 kutokana na michango ya wanachama ikiwa ni sawa na ongezeko
la asilimia 21.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 188.1 zilizokusanywa mwaka 2011.
Ongezeko hili lilitokana na waajiri kuzingatia sheria kwa kuleta michango kwa wakati
na uandikishaji wa wanachama wapya. Aidha, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 180,049
mwaka 2011 hadi 203,981 mwaka 2012. Mfuko pia ulilipa mafao ya jumla ya shilingi bilioni
99.4. Mafao hayo ya PPF yalijumuisha na mafao ya elimu ambayo hulipwa kwa ajili ya
kusomesha watoto wasiozidi wanne wa mwanachama aliyefariki akiwa kazini. Mwaka 2012
mfuko ulisomesha watoto 1,333 kwa gharama ya shilingi milioni 683 ikilinganishwa na
watoto 1,392 waliosomeshwa mwaka 2011 kwa gharama ya shilingi milioni 573. Watoto
hawa husomeshwa kuanzia elimu ya chekechea hadi kidato cha nne.
40.
Mheshimiwa Spika, mapato yatokanayo na uwekezaji yaliongezeka kutoka shilingi bilioni
91.4 mwaka 2011, hadi kufikia shilingi bilioni 105.5 kwa mwaka 2012 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 15.4. Aidha, thamani ya Mfuko kufikia Desemba 2012, ilikuwa imeongezeka
kufikia shilingi bilioni 1,089.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.8 ikilinganishwa
na thamani ya Mfuko ya shilingi bilioni 894.5 ilivyokuwa Desemba 2011.
41.
Mheshimiwa Spika, Mfuko unatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 281.7, kuandikisha
wanachama wapya 72,000 kutoka sekta ya umma na binafsi, na kukusanya shilingi bilioni
125.6 kutokana na uwekezaji ifikapo Desemba 2013. Aidha, thamani ya Mfuko inatarajiwa
kufikia shilingi bilioni 1,302.68.
42. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo
na changamoto kadhaa katika Mifuko ya Hifadhi ya jamii ikiwemo: Wanachama kulalamikia
kiwango kidogo cha mafao kitolewacho na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pale
wanapostaafu. Vile vile, kuna suala la malimbikizo ya madeni yanayotokana na Mifuko
kugharimia utekelezaji wa miradi ya Serikali. Aidha, katika kutafuta ufumbuzi wa
changamoto hizo Serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii imepanga
kutathmini uwezo wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kupendekeza viwango vya mafao;
na kuhakikisha kwamba, mifuko hiyo inakuwa endelevu. Vile vile, Serikali inaendelea
kulipa madeni ya mifuko ya jamii kwa awamu na pia imeunda kamati ya kuchambua na
kuhakiki madeni mengine ya baadhi ya mifuko ili kupendekeza njia endelevu ya kuyalipa.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania - TRA
43. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imeendelea kutekeleza Mpango wa tatu wa Maboresho wa mwaka 2008/09 - 2012/13
ambao umekuwa msingi wa kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Katika
jitihada za kuongeza mapato ya ndani, Wizara kupitia TRA imetekeleza yafuatayo: kuanzisha
mfumo wa kimtandao wa kuwasilisha ritani za kodi - tax returns; kufanya tathmini ya
maeneo hatarishi katika Utawala wa Sekta za Umma; kuweka mfumo wa taarifa wa RADDEX
2 na kutoa mafunzo kwa watumiaji; kusambaza Mfumo wa Ki-elektroniki wa Ufuatiliaji
Usafirishaji Mizigo (Electronic Cargo Tracking System); na kuboresha mfumo wa utunzaji
kumbukumbu na Taarifa za Magari. Aidha, TRA imekamilisha uandaaji wa Awamu ya Nne
ya Mpango wa Maboresho (2013/14 - 2017/18) unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika
mwaka wa fedha 2013/14.
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2013/14, Wizara kwa kushirikiana na TRA itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa makusanyo na kuchukua hatua mbalimbali za kisera
na kiutawala katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi.
45. Mheshimiwa
Spika, mnamo mwezi Mei 2013 kulitokea tatizo la mlundikano wa makonteina Bandarini
Dar es Salaam kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kuyaondoa. Kutokana na tatizo
hili Wizara ilikutana na wadau wote pamoja na wafanyabiashara ili kuondoa adha hiyo.
Katika kikao hicho Mamlaka ya Mapato ilielekezwa kushughulikia suala hilo kulingana
na sheria na taratibu ili wafanyabiashara waweze kulipia makonteina yao na kuyaondoa
bandarini. Tunapenda ieleweke kwamba katika tatizo hili hakuna kodi yoyote iliyoongezwa
kwa makonteina hayo ya wafanyabiashara na walitakiwa kulipa kodi stahili. Huduma
za Kibenki Benki Kuu ya Tanzania
46. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2012/13, Wizara kwa kupitia Benki Kuu imeendelea kutekeleza mabadiliko
chanya katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachochea maendeleo
ya jamii na ukuaji wa uchumi. Mabadiliko ya sekta ya fedha yamesababisha utendaji
mzuri wa Taasisi za Fedha ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya mabenki kutoka
benki 49 mwezi Februari, 2012 mpaka benki 51 mwisho wa mwezi Februari 2013. Aidha,
rasilimali za mabenki zimeimarika zaidi na kufikia shilingi trilioni 17.3 mwezi Februari
ambapo mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imefikia shilingi trilioni 8.8.
47.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na jitihada za kuboresha upatikanaji wa mikopo,
Benki Kuu imeanzisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za wakopaji (Databank)
na utaratibu wa utoaji wa taarifa za wakopaji kwa kutumia kampuni binafsi (Credit
Reference Bureaux). Mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za wakopaji umeshaanza
kufanya kazi na mabenki yameshaanza kupeleka taarifa za wakopaji. Kampuni mbili za
utoaji wa taarifa za wakopaji zimeshapewa leseni na wapo katika maandalizi ya mwisho
ili waanze kutoa huduma ya kutoa taarifa hizo. Mfumo huu utaboresha upatikanaji wa
mikopo ya muda wa kati na muda mrefu.
48. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Benki Kuu imetoa Mwongozo wa Huduma za Kibenki kwa Kutumia Wakala wa Mwaka
2013 (Guidelines on Agent Banking for Banking Institutions, 2013) ambao ulianza kutumika
mwezi Februari, 2013. Kutolewa kwa mwongozo huu ni sehemu ya mpango wa kuweka mazingira
yatakayowezesha kupanua wigo wa huduma za kibenki na kuhakikisha usalama wa benki
mbalimbali zitakazojihusisha na mfumo wa utoaji huduma za kibenki kwa kutumia mawakala.
Mfumo huu utarahisisha upatikanaji wa huduma bora na nafuu za kibenki.
49.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imeunda Kamati ya Kitaifa ya Uthabiti wa
Mfumo wa Fedha (Tanzania Financial Stability Forum) ili kusaidia kuimarisha ushirikiano
na kubadilishana taarifa kati ya wadhibiti wa sekta ya fedha kama msingi imara kwa
ajili ya kuhakikisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini na kupanua wigo wa usimamizi
katika mfumo wa fedha kutoka usimamizi unaolenga taasisi moja moja kwenda usimamizi
wa mfumo wa fedha unaolenga sekta nzima ya fedha kwa ujumla wake. Aidha, taarifa inayoonesha
hali halisi ya uthabiti wa sekta ya fedha inatolewa kila baada ya miezi sita.
50.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu za Afrika Mashariki zilikubaliana kutengeneza mfumo wa
malipo utakaorahisisha malipo kwa kutumia sarafu za nchi husika. Mfumo huu ujulikanao
Kama East African Cross Border Payment System - EAPS, umefikia hatua ya majaribio
kupitia mifumo ya Malipo Makubwa (Real Time Gross Settlement System – RTGS) ya nchi
za Tanzania, Kenya na Uganda. Mategemeo ni mfumo huu kuanza kutumika kwa nchi hizi
tatu, ikiwa taratibu zote za kujiunga na mfumo huu zitakuwa zimekamilika, mwezi Julai
2013. Aidha, Nchi za Rwanda na Burundi zitakapokuwa tayari zitajiunga na mfumo huo.
Kuanza kwa mfumo huu wa malipo kutarahisisha malipo katika Jumuiya na kukuza shughuli
za kibiashara na uchumi.
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2013/14, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu itaandaa mapendekezo ya kutunga Sheria
ya kusimamia mifumo ya malipo nchini (National Payment Systems Act). Aidha, Benki
kuu itaendelea kuandaa sera za kifedha na kusimamia utekelezaji wake. Vile vile, Wizara
kwa kushirikiana na Benki Kuu itafanya tathmini ya mpango wa utekelezaji wa Awamu
ya Pili ya Mpango wa Maboresho ya Sekta ya Fedha unaoishia Juni, 2013 na kuandaa
mpango wa utekelezaji wa awamu ya tatu. Kadhalika, Benki Kuu itahakikisha mwongozo
wa kitaifa kuhusu elimu ya masuala ya fedha (Financial Education Framework) unazingatiwa.
Mwongozo huu unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kutumia
huduma za fedha katika shughuli zao za kila siku.
Benki ya Maendeleo TIB -
TIB Development Bank
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 Benki
ya Rasilimali (TIB) iliendelea na utekelezaji wa marekebisho ili kuwa benki imara
ya maendeleo tangu Novemba 2012 benki ilibadilisha jina na kuitwa TIB Development
Bank ili kuweka wazi dhana ya benki ya maendeleo. Aidha, mchakato wa uanzishwaji wa
benki ambayo kampuni tanzu inayojishughulisha na shughuli za biashara (TIB Corporate
Bank) ambapo usajili wake upo katika hatua za mwisho. Mara taratibu zote zitakapokamilika,
TIB itafanya kazi katika mfumo wa makampuni mawili yanayotegemeana moja likijikita
kwenye shughuli za maendeleo (TIB Development Bank) na lingine kwenye shughuli za
kibiashara (TIB Corporate Bank). Benki hizi zitakamilisha muundo wake ifikapo mwezi
Septemba, 2013.
53. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13,
Benki ilifungua tawi mkoani Mbeya na ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hii
inafanya benki kuwa na jumla ya matawi matano na ofisi tatu za kanda. Aidha, hadi
kufikia Desemba 2012, Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 242.9
ikilinganishwa na mikopo ya shilingi bilioni 181.7 Desemba 2011 sawa na ongezeko la
asilimia 74.8. Mikopo mingi ilitolewa kwenye sekta ya kilimo na usindikaji wa mazao
ya kilimo (mikopo hii ni tofauti na ile ya Dirisha la kilimo). Vile vile, mtaji wa
benki ulifikia shilingi bilioni 142.1 baada ya Serikali kuongeza shilingi bilioni
40. Benki ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 8.6 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 48 toka shilingi bilioni 5.8 zilizopatikana mwaka ulioishia Desemba 2011.
54. Mheshimiwa Spika, Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo
TIB liliendelea kutoa mikopo kwa wakopaji mbalimbali kwa riba nafuu. Tangu kuanza
kwa dirisha mwaka 2010 hadi kufikia Desemba 2012, maombi yenye thamani ya shilingi
bilioni 40.1 yaliidhinishwa ambapo shilingi bilioni 20.0 (asilimia 49.9) zilikopeshwa
kwa makampuni; shilingi bilioni 5.7 (asilimia 14.2) kwa taasisi ndogo za fedha zinazokopesha
wakopaji wadogo; na shilingi bilioni 14.4 (asilimia 35.9) kwa vikundi vya kuweka na
kukopa (SACCOS) ambavyo pia vinafaidisha wakopaji wadogo. Hii inamaanisha asilimia
50.1 ya mikopo imetolewa kwa wajasiriamali wadogo. Aidha, kuanzia Julai, 2013 Dirisha
la Kilimo lililopo TIB litahamishiwa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
55.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba 2013, mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo
TIB katika sekta mbalimbali inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 379.2 na faida kabla
ya kodi inatarajiwa kufikia shilingi bilioni 16.6.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
- TADB
56. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na utekelezaji wa Mpango
Kazi wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB. Lengo la kuanzisha
benki hiyo ni kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu katika sekta ya kilimo
inayojumuisha uvuvi na mifugo. TADB ilisajiliwa BRELA chini ya Sheria ya Kampuni ya
mwaka 2002 kwa jina la Tanzania Agricultural Development Bank Limited (TADB Ltd).
Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 90.0 kati ya lengo la shilingi bilioni 100 kimeshatolewa
kama kianzio cha Mtaji. Vile vile, Muundo wa benki ya kilimo na majukumu ya wafanyakazi
katika nafasi mbalimbali umeandaliwa. Mwenyeketi na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi
wameteuliwa na ajira za maafisa waandamizi wa benki hiyo inatarajiwa kukamilika hivi
karibuni. Katika mwaka 2013/14, shilingi bilioni 10 zimetengwa ili kukamilisha lengo
la mtaji wa kuanzia wa shilingi bilioni 100.
Twiga Bancorp 57.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi kinachoishia Desemba 2012 Taasisi iliendelea kupanua
shughuli zake kwa kufungua tawi moja mkoani Dodoma na kuifanya taasisi kuwa na matawi
matano. Katika kipindi hicho, amana za wateja zilifikia shilingi bilioni 58.41 ikilinganishwa
na shilingi bilioni 54.2 Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 7.8. Aidha, mikopo
iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 39.43 ikilinganishwa na shilingi bilioni 35.9
kwa mwaka ulioishia Desemba 2011 sawa na ongezeko la asilimia 9.8. Vile vile, Taasisi
iliwekeza shilingi bilioni 4.7 kwenye Dhamana za Serikali na Amana katika Benki zingine
ikilinganishwa na shilingi bilioni 19.0 zilizowekezwa katika kipindi kama hicho mwaka
2011.
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka unaoishia Desemba, 2013,
amana za wateja zinatarajiwa kufikia shilingi bilioni 73.25 kutoka shilingi bilioni
58.41 za Desemba, 2012; mapato kutokana na shughuli mbalimbali za kibiashara yanatarajia
kufikia shilingi bilioni 12.66 ikilinganishwa na shilingi bilioni 9.56 zilizokusanywa
Desemba, 2012; na mtaji ghafi wa Benki (Owners’ Equity) unatarajiwa kukua kutoka shilingi
bilioni 5.81 hadi shilingi bilioni 7.24 ifikapo Desemba 2013. Aidha, thamani ya mikopo
kwa wateja inatarajia kufikia shilingi bilioni 49.10 na uwekezaji katika Dhamana za
Serikali na Amana za Muda Maalum kwenye mabenki unatarajia kufikia shilingi bilioni
16.80. Vile vile, Taasisi inatarajia kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni
0.48.
Benki ya Posta - TPB
59. Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha mwaka 2012 Benki ilianzisha huduma mpya ya Platinum Account inayolenga vijana
walio katika Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine za elimu ya juu. Manufaa ya huduma hii
ni kuwawezesha vijana kujiwekea akiba na kupitishia mikopo ya elimu. Aidha, Benki
iliendelea kupanua mtandao wake kwa kufungua matawi madogo katika ngazi ya Wilaya
katika vituo vya Shirika la Posta. Vile vile, Benki ilianzisha huduma ya POPOTE Quick
Account, inayomuwezesha mteja kupata huduma za benki mahali popote kupitia simu ya
mkononi kwa lengo la kuwafikia Wananchi walio wengi wanaoishi vijijini.
60.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, amana za wateja zimeongezeka kutoka shilingi
bilioni 120.92 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 144.56 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 19.4. Aidha, benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 103.34
ikilingalishwa na shilingi bilioni 66.75 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia
54.83. Vile vile, uwekezaji katika vitega uchumi vya Benki ya Posta umeongezeka kutoka
shilingi bilioni 117.67 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi bilioni 146.96, ikiwa ni
ongezeko la asilimia 24.9. Kadhalika, Benki imepata faida baada ya kodi ya shilingi
bilioni 3.59 ikilinganishwa na shilingi bilioni 2.58 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 39.4. Katika mwaka 2012/13, Serikali iliiongezea Benki ya Posta mtaji
wa shilingi bilioni 1.5 na kufanya mtaji wa benki kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.82.
61.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, benki itaendelea na mkakati wake wa kuimarisha
huduma zitolewazo kupitia Shirika la Posta kwa kukarabati na kuunganisha katika mtandao
wa benki vituo 10 vya Posta vilivyoko Temeke, Tunduma, Kahama, Geita, Masasi, Peramiho,
Njombe, Kyela, Simiyu na Kasulu hivyo kuvipa uwezo wa kutoa huduma za haraka. Vituo
hivi vitakuwa ni matawi madogo na hivyo kufanya benki kufikisha jumla ya matawi 23.
Aidha, benki itafunga vifaa vya ki-elektroniki katika vituo vya mauzo. Vile vile,
Benki inatarajia kupanua wigo wa mikopo kwa kuingia mikataba na Sekretarieti za Mkoa
na Jeshi la Kujenga Taifa, na kuongeza kipindi cha marejesho kutoka miaka mitatu hadi
minne. Kadhalika, Benki inatarajia kupata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni
5.11 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.5 ikilinganishwa na faida ya shilingi bilioni
4.07 iliyopatikana mwaka 2012.
Taasisi za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
62.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara iliendelea kusimamia taasisi
za kitaalam na huduma nyinginezo ambazo ziko chini ya Wizara ya Fedha ambazo ni Ofisi
ya Taifa ya Takwimu – NBS; Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi – NBAA; Bodi ya Wataalamu
wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB; na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha. Aidha, huduma nyingine
zinajumuisha: Usimamizi wa shughuli za Bima; Masoko ya Mitaji na Dhamana; na huduma
za dhamana ya uwekezaji.
Taasisi za Mafunzo
63. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara imeendelea kusimamia taasisi za mafunzo zilizo
chini yake. Taasisi hizo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM, Taasisi ya Uhasibu
Arusha – IAA, Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini
– IRDP, na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC .
CHANGAMOTO 64.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto
kadhaa zikiwemo zifuatazo:-
i) Kudhibiti matumizi ya fedha
za umma sambamba na kuongeza mapato ya Serikali;
ii) Kuzingatia
kanuni na taratibu zilizoainishwa kwenye Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA)
na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wafadhili wa nje; iii) Kuwa na Sera
ya Mali ya Serikali.
iv) Kufikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi;
v) Kuwepo kwa mahitaji makubwa ya fedha
nje ya bajeti;
vi) Kuwepo kwa mchakato mrefu wa upatikanaji wa
fedha za kugharamia Miradi ya Maendeleo hasa mikopo ya kibiashara (non-conscessional
borrowing); na
vii) Kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani
katika mafungu mbalimbali ambayo yameshindwa kuingizwa kwenye viwango vya bajeti.
65. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara
itachukua hatua kupitia mipango na bajeti zake ili kuhakikisha kuwa changamoto hizi
zinapatiwa ufumbuzi katika mwaka 2013/14 na kuendelea. Hatua za ufumbuzi wa changamoto
hizi zitaelezwa katika hotuba ya bajeti ya Serikali itakayowasilishwa Juni 13, 2013.
Mapitio
ya Mapato na Matumizi ya Mafungu ya Wizara kwa Mwaka 2012/13
66. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, majukumu ya Wizara yalitekelezwa katika mafungu
sita ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya
Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 -
Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu; na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha,
Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, linaombewa fedha Bungeni na Waziri wa Fedha
kwa mujibu wa Sheria.
Fungu 50 – Wizara ya Fedha
67. Mheshimiwa
Spika, Wizara ilitarajia kupata shilingi bilioni 124.42 kutoka vyanzo mbalimbali
vya mapato yasiyo ya kodi kupitia Fungu 50. Vyanzo hivyo ni pamoja na mauzo ya mali,
uuzaji wa nyaraka za zabuni na mapato kutoka katika Mashirika ya Umma na Taasisi za
Serikali yakiwemo Gawio, Michango na Marejesho ya mikopo. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, makusanyo yalifikia shilingi bilioni 37.27 sawa na asilimia 29.97 ya lengo.
Makusanyo zaidi yanatarajiwa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha baada ya Mashirika
mengi kuandaa hesabu za mwaka na ukaguzi wa hesabu hizo kukamilishwa.
68.
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 50 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi
bilioni 98.41 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 546.51 kwa ajili
ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 70.32 sawa na asilimia 71.46 ya makadirio na matumizi ya maendeleo
yalifikia shilingi bilioni 311.28 sawa na asilimia 56.96 ya makadirio.
Fungu
23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
69. Mheshimiwa Spika, makadirio
ya matumizi ya Fungu 23 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi bilioni 75.12 kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 6.12 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 49.34
sawa na asilimia 65.67 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni
1.29 sawa na asilimia 21.05 ya makadirio.
Fungu 22 - Deni la Taifa
70.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13 makadirio ya matumizi ya Fungu 22
yalikuwa shilingi bilioni 2,735.91. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013 matumizi ya fungu
hili yalifikia shilingi bilioni 2,226.70 sawa na asilimia 81.39 ya makadirio.
Fungu
21- HAZINA
71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiria kukusanya mapato ya shilingi bilioni
8,070. Hadi kufikia Aprili, 2013, TRA ilikusanya shilingi bilioni 6,580 sawa na asilimia
97.84 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 6,725 katika kipindi hicho.
72.
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 21 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi
bilioni 725.57 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 101.95 kwa ajili
ya matumizi ya maendeleo. Aidha, kiasi cha Shilingi bilioni 50.66 kilifanyiwa uhamisho
kuongezea katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na kufanya makadirio ya matumizi
ya maendeleo kwa mwaka 2012/13 kuwa shilingi bilioni 152.61. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 516.61 sawa na asilimia 71.2
ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 131.95 sawa na asilimia
86.46 ya makadirio.
Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu
73.
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi ya Fungu 13 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi
bilioni 2.16 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 0.26 kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia
shilingi bilioni 1.01 sawa na asilimia 46.62 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo
yalifikia shilingi bilioni 0.04 sawa na asilimia 14.72 ya makadirio.
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
74. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi
ya kawaida kwa Fungu hili yalikuwa shillingi bilioni 1.99, hadi kufikia Aprili, 2013
matumizi yalifikia shilingi bilioni 1.33 sawa na asilimia 66.83 ya makadirio.
Fungu
45- Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
75. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi
ya Fungu 45 kwa mwaka 2012/13 yalikuwa shilingi bilioni 55.02 kwa ajili ya matumizi
ya kawaida na shilingi bilioni 9.62 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia
mwezi Aprili, 2013, matumizi ya kawaida yalifikia shilingi bilioni 39.51 sawa na asilimia
71.81 ya makadirio, na matumizi ya maendeleo yalifikia shilingi bilioni 3.18 sawa
na asilimia 33.0 ya makadirio.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA
FEDHA 2013/14
76. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14,
majukumu ya Wizara yatatekelezwa katika mafungu saba ya kibajeti. Mafungu hayo ni
Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 23 - Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali; Fungu 22
- Deni la Taifa; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 13 - Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu;
na Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha na Fungu 7- Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Aidha, Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo inajitegemea litaendelea kuombewa
fedha Bungeni na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sheria.
Mapato 77.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ya Fedha inakadiria kukusanya
mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi 2,718,102,000 (bilioni 2.72) kupitia Fungu
50 - Wizara ya Fedha na shilingi 124,013,512,000 (bilioni 124.01) kupitia Fungu 7-
Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Maombi ya Fedha 78. Mheshimiwa
Spika, baada ya kueleza kwa kina utekelezaji wa majukumu na kazi za Wizara kwa mwaka
2012/13 na mpango na malengo ya bajeti kwa mwaka 2013/14, sasa napenda kuwasilisha
rasmi mapendekezo ya maombi ya fedha kwa mwaka 2013/14 kwa ajili ya matumizi ya Fungu
50, 23, 22, 21, 13, 10, 7, na 45 kama ifuatavyo:-
Fungu 50 – Wizara ya Fedha 79.
Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 53,011,091,000
(bilioni 53.01). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 4,564,609,000 (bilioni 4.56) na
matumizi mengineyo shilingi 48,446,482,000 (bilioni 48.45).
(b) Miradi ya
Maendeleo Shilingi 233,669,169,000 (bilioni 233.67). Kati ya hizo:-
(i)
Fedha za Ndani - Shilingi 10,200,000,000 (bilioni 10.20).
(ii) Fedha za
Nje - Shilingi 223,469,169,000 (bilioni 223.47).
Fungu 23 – Idara ya Mhasibu
Mkuu wa Serikali: 80. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi 80,831,672,000 (bilioni 80.83). Kati ya hizo Mishahara
shilingi 4,434,410,000 (bilioni 4.43) na matumizi mengineyo shilingi 76,397,262,000
(bilioni 76.40).
(b) Miradi ya Maendeleo – Shilingi 4,755,547,000
(bilioni 4.76) Kati ya hizo:- (i) Fedha za Ndani -Shilingi 400,000,000
(bilioni 0.40).
(ii) Fedha za Nje -Shilingi 4,355,547,000 (bilioni 4.36).
Fungu
22- Deni la Taifa 81. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 3,319,017,772,000
(bilioni 3,319.02). Kati ya hizo Mishahara ni shilingi 6,311,772,000 (bilioni 6.31)
na matumizi mengineyo ni shilingi 3,312,706,000,000 (bilioni 3,312.71).
Fungu
21 - HAZINA: 82. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida Shilingi 1,378,142,566,000 (bilioni 1,378.14). Kati ya hizo mishahara
ni shilingi 2,632,424,000 (bilioni 2.63) na matumizi mengineyo shilingi 1,375,510,142,000
(bilioni 1,375.51) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini
ya Fungu hili, nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.
(b)
Miradi ya maendeleo ni shilingi 38,190,162,000 (bilioni 38.19). Kati ya hizo:-
(i)
Fedha za Ndani- Shilingi 7,893,000,000 (bilioni 7.89)
(ii) Fedha za
Nje- Shilingi 30,297,162,000 (bilioni 30.30)
Fungu 13 – Kitengo cha
Udhibiti wa Fedha Haramu: 83. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa
mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi 1,944,790,000 (bilioni 1.94).
(b)
Miradi ya Maendeleo, fedha za nje Shilingi 399,985,000 (bilioni 0.39).
Fungu
10 – Tume ya Pamoja ya Fedha: 84. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa
mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,064,424,000
(bilioni 2.06) kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi 362,771,000 (bilioni
0.36) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 1,701,653,000 (bilioni 1.70) ni matumizi
mengineyo. Fungu 7 – Ofisi ya Msajili wa Hazina: 85. Mheshimiwa
Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya kawaida - Shilingi
38,088,142,000 (bilioni 38.08). Kati ya hizo shilingi 303,192,000 (bilioni 0.30)
ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 37,784,950,000 (bilioni 37.78) ni matumizi mengineyo.
(b)
Miradi ya Maendeleo - Shilingi 1,665,300,000 (bilioni 1.67) Kati ya hizo:-
(i)
Fedha za Ndani -Shilingi 600,000,000 (bilioni 0.60).
(ii) Fedha za Nje -Shilingi
1,065,300,000 (bilioni 1.07).
Fungu 45: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi 86.
Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha fedha kama ifuatavyo:-
(a) Matumizi ya kawaida shilingi 57,406,414,000
(bilioni 57.40). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 6,692,935,000 (bilioni 6.69)
na matumizi mengineyo shilingi 50,713,479,000 (bilioni 50.71).
(b) Miradi ya
maendeleo shilingi 21,449,100,000 (bilioni 21.45), kati ya hizo:-
(i)
Fedha za ndani shilingi 15,250,000,000 (bilioni 15.25).
(ii) Fedha
za nje shilingi 6,199,100,000 (bilioni 6.20).
HITIMISHO 87.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba
ya bajeti ya Wizara inapatikana katika tovuti ya Wizara () Aidha, naomba hotuba kama
ilivyo kwenye kitabu iingizwe kwenye “Hansard”.