Kanisa Barani Afrika halina budi kuanza mchakato wa kulitegemeza Kanisa
Kanisa Barani Afrika linakabiliwa na changamoto ya kulitegemeza Kanisa ili liweze
kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima:
kiroho na kimwili. Ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali
watu, vitu na fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia, kwa kutambua
kwamba, ujenzi wa Kanisa la Afrika unawategemea zaidi Waafrika wenyewe.
Umefika
wakati kwa waamini Barani Afrika kujenga moyo na ari ya kujiamini katika majukumu
yao ndani ya Kanisa na kuondokana na kasumba ya kutegemea misaada kutoka nje ya Bara
la Afrika kwani hali imebadilika na wanapaswa kusoma alama za nyakati.
Ni
changamoto na mwaliko uliotolewa hivi karibuni na Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki
la Machakos, Kenya wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kisasa la Parokia
ya Mitaboni, Jimboni humo. Kiasi cha shilingi za Kenya millioni 1.6 zilikusanywa kutoka
kwa waamini na wananchi wenye mapenzi mema walioshiriki katika harambee hii.
Askofu
Kivuva anasema kwamba, ikiwa kama waamini watamegemea Mwenyezi Mungu na kumwendea
kwa kwa sala na unyenyekevu anaweza kutenda miujiza, kiasi cha kuwashangaza. Ameipongeza
Familia ya Mungu Parokiani hapo kwa kujitoa kimasomaso kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.
Kanisa nchini Kenya litaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kwamba, Serikali
isaidie kuchangia upatikanaji wa waalim ili Kenya iweze kucharuka kwa maendeleo katika
sekta ya elimu.
Askofu Kivuva amefanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi millioni
2.3 kwa ajili ya Ujenzi wa Seminari ndogo ya Papa Paulo VI, iliyoko Katoloni, Jimboni
Machakos. Jumuiya ndogo ndogo zimehusishwa kikamilifu katika mchakato wa kulitegemeza
Kanisa kuanzia katika ngazi mbali mbali hadi kufikia kilele chake kwa Siku ya Tegemeza
Jimbo, inayowakusanya waamini wa Parokia na Taasisi zote za Kanisa husika.