2013-06-06 07:54:53

Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo, umoja, amani na mshikamano!


Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwa Mwaka 2013 yamekuwa na uzito wa pekee kutokana na Mama Kanisa kuendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, changamoto kwa Waamini kumshuhudia Kristo katika maisha na vipaumbele vyao. Ni tukio ambalo limewaunganisha Wakatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia chini ya Baba Mtakatifu Francisko kuabudu Ekaristi Takatifu kwa wakati mmoja.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha hija ya maisha ya Wakristo, wanaoitwa na kukusanywa na Kristo kwa ajili ya kujenga na kuliimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni mwaliko wa kushiriki na kujenga: misingi ya haki, amani na upatanisho; umoja na mshikamano mambo yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni meza ya Neno la Mungu na chakula cha maisha ya uzima wa milele, changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanaishi katika neema ya utakaso na kifungo cha upendo.

Ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, iliyoshuhudia watoto 917 kutoka Dekania ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba wakipokea Komunio ya kwanza kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, Jimbo Katoliki Dodoma.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuendelea kuwa ni mashahidi wa amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wanaowazunguka. Askofu Nyaisonga amewataka watanzania kwa ujumla kudumisha misingi ya amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Wanandoa wadumishe tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; watekeleze wajibu na dhamana ya malezi na elimu kwa watoto wao.

Waamini wa Dekania ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Katoliki Dodoma walitoka kwa maandamano na nyimbo, kuelekea kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, hapo wakakusanyika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hili ni tukio ambalo wanasema wachunguzi wa mambo limeacha guzmo la pekee mjini Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.