Utajiri unaofumbatwa katika Sinodi za Maaskofu Kimabara
Idara ya uchapaji ya Vatican (LEV) hivi karibuni imechapisha kazi kubwa ya ushauri
uliotolewa na Mababa wa Sinodi za Kimabara na kuhaririwa na Askofu mkuu Nikola Eterovic,
Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu kwa kutambua kwamba, Mama Kanisa yupo kwa ajili
ya Kuinjilisha na kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa watu wa
nyakati zote.
Kitabu hiki
ni matunda ya kazi ya ushauri uliotolewa na Mababa wa Sinodi za Maaskofu kuanzia mwaka
2004 hadi mwaka 2012. Kwa maneno mengine, hizi ni Sinodi ambazo zimesimamiwa kwa namna
ya pekee na Askofu mkuu Nikola Etrovic tangu alipopewa dhamana hii na Mwenyeheri Yohane
Paulo wa Pili.
Huu ni utajiri wa maisha na utume wa Kanisa mahalia kutoka
sehemu mbali mbali za dunia; unaoonesha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu
Petro katika utekelezaji wa shughuli na mikakati ya kiuchungaji kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa la kiulimwengu. Umuhimu na haja ya Uinjilishaji Mpya ni changamoto
iliyotolewa kwa namna ya pekee kabisa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
miaka 50 iliyopita.
Mapapa waliofuata walianza kuweka mikakati ya shughuli
za kichungaji ili kubainisha mbinu ambazo Kanisa lingeweza kutumia katika kutekeleza
wajibu huu msingi ambao Kristo mwenyewe ameliachia Kanisa lake. Maadhimisho ya Sinodi
za Maaskofu imekuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kuweza kusali, kutafakari na kushirikishana
uzoefu, mang’amuzi na vipaumbele kutoka kwa Makanisa mahalia.
Bado Kanisa linatumwa
kutangaza Habari Njema kwa watu ambao hawajapata fursa ya kusikia Injili ya Kristo,
lakini pia Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linaendelea kuchangamotishwa
na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kufanya Uinjilishaji Mpya kwa kusoma alama za nyakati
pamoja na kuwasaidia wale ambao kutokana na sababu mbali mbali wamelegea katika imani
na maisha ya Kikristo, ili waweze kuuona tena Mlango wa Imani ambao ni Kristo ambaye
ni njia, ukweli na uzima na kuishi mintarafu Mafundisho na Kweli za Kiinjili.
Hadi
sasa kuna Sinodi kumi na mbili ambazo zimekwisha adhimishwa hapa mjini Vatican kwa
ajili ya Makanisa mahalia na baadaye kufuatiwa na Nyaraka za Kichungaji kutoka kwa
Mababa Watakatifu. Washauri wa Sinodi za Maaskofu wana nafasi maalum katika Maadhimisho
ya Sinodi ya Maaskofu: Wao wanafanya maandalizi ya kina katika Maadhimisho ya Sinodi
kwa kuandaa hati elekezi inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Lineamenta” inafuatiwa
na hati ya kutendea kazi “Instrumentum Laboris” ambayo kimsingi ni mkusanyiko wa mawazo
mbali mbali yanayogusa masuala ya kichungaji, kitaalimungu na kikanisa.
Kitabu
hiki ambacho kina utajiri mkubwa, kinaonesha hotuba zilizotolewa na Askofu mkuu Nikola
Etrovic wakati wa maadhimisho ya Sinodi hizi. Kuna hotuba za Papa Yohane Paulo wa
Pili na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Sinodi za Maaskofu zimekuwa
ni nyenzo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Zimesaidia kuvumbua utajiri
wa historia, maisha na utume wa Kanisa Katoliki kutoka kila pembe ya dunia, kama sehemu
ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya anasema Askofu mkuu Nikola Etrovic.