2013-06-05 07:56:41

Uhakika wa usalama wa chakula ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akishiriki kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili kuhusu malengo ya maendeleo endelevu hivi karibuni, amekazia umuhimu wa usalama wa chakula na lishe; upandaji wa miti na utunzaji bora wa mazingira kama njia ya kudhibiti ukame. RealAudioMP3

Anasema kwamba, inasikitisha kuona kuwa hata katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia bado kuna watu wanaoteseka kwa baa la njaa sehemu mbali mbali duniani. Uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa. Baa la njaa limeendelea kuwa ni chanzo kikuu cha vifo vya watu wengi duniani, hususan kutoka katika nchi zinazoendelea duniani.

Ukosefu wa chakula na lishe bora ni tatizo la kimaadili na utu wema ambalo linachangiwa na sera tenge zinazoongoza soko huria; uchu na uroho wa mali na utajiri wa haraka haraka; baadhi ya mazao ya nafaka kutumika kama nishati uoto; upotevu wa chakula kinachomwagwa kutokana na matumizi mabaya pamoja na nchi changa kushindwa kujiunga na soko la kimataifa kutokana na ukiritimba na vikwazo visivyo na msingi.

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, inapambana kufa na kupona na baa la njaa na lishe duni, kwani chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, hivyo hakipaswa kushughulikiwa kama bidhaa nyingine katika soko. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuibua mbinu mkakati utakaoiwezesha kuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na lishe bora kwa mamillioni ya watu duniani wanaoendelea kuteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Jambo hili linawezekana ikiwa kama wahusika wakuu wanaoteseka na njaa watashirikishwa kikamilifu. Mambo yanayosababisha njaa na utapiamlo yanapaswa kubainishwa na kushughukiwa kikamilifu kwa kutenga rasilimali ya kutosha, jambo linalohitaji utashi wa kisiasa, moyo na ari ya mshikamano wa dhati kutoka kwa wadau mbali mbali. Ushirikiano huu utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupambana na baa la njaa duniani.

Fedha, teknolojia, pembejeo na utaalam wa kilimo bora ni mambo msingi sanjari na kuhakikisha kwamba, kuna mikakati makini katika kuzalisha, kusafirisha na kugawa mazao haya ili yaweze kuwafikia walaji kwa wingi na ubora unaotakiwa. Mikakati ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia na baadaye inapaswa kujielekeza kutafuta mbinu za kupambana na baa la njaa katika uso wa dunia, kwani hii ni sehemu ya haki msingi za binadamu.

Mchakato wa kutaka kuwa na uhakika wa usalama wa chakula hauna budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira na kilimo cha kisasa. Umilikaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa baadhi ya watu ndani ya Jamii linaweza kuwa ni tatizo kubwa kwa siku za usoni, changamoto kwa wanasiasa na watunga sera kuongozwa na dhamiri nyofu wanapotekeleza dhamana hii nyeti katika maisha ya watu wao! Jamii inapaswa kuwekeza katika familia na kwa wakulima wadogo wadogo ili waweze kushiriki katika mchakato wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Vyama vya ushirika vinaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili kuongeza tija na uzalishaji. Jumuiya ya Kimataifa ibainishe programme zinazoweza kuwasaidia wakulima kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, mambo yanayochangia kukwamisha maendeleo ya watu.

Dunia ambayo watu wengi wana itamani kwa sasa na kwa siku za usoni ni ile isyokuwa na baa la njaa wala utapiamlo! Jambo hili linawezekana ikiwa kama kila mtu atatekeleza wajibu wake anasema Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.