Yaliyojiri kwenye rasimu ya muswada wa Katiba Mpya ya Tanzania
Mambo ambayo hayakuingizwa kwenye muswada wa Katiba Mpya ni pamoja na: Serikali za
majimbo, mahakama ya kadhi, wakuu wa mikoa na wilaya, serikali za mitaa pamoja na
uraia wa nchi mbili. Ifuatayo ni hotuba ya Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania wakati wa uzinduzi wa Rasimu ya Katiba Mpya
ya Tanzania.
UTANGULIZI Ndugu Wananchi,
Awali ya yote namshukuru
mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya leo ya kuzindua Rasimu ya Katiba.
pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria halfa hii ikiwa ni mwendelezo wa mchakato
muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa mabadiliko Februari, 2012. Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83).
Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Tume imepewa miezi kumi na minane kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi
rasmi ambayo ilikuwa Mei 2, 2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu
yake. Kufuatana na ratiba hiyo Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika
kipindi cha miezi mitano kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi hiyo ilifanywa
kama tulivyopanga. Tume ilijigawa katika makundi na ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume
ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati
ya hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi.
Tume pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje ya nchi kwa njia mbali mbali
kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu maalum za Tume, barua kupitia Masanduku ya Barua
ya Tume, Mitandao ya Kijamii ya barua pepe; facebook ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala
mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi wa simu.
Tume ilitumia mwezi
Januari, 2013 kukusanya maoni ya makundi mbali mbali katika jamii, ikiwa ni pamoja
na vyama vya siasa, taasisi za Serikali, taasisi za dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi,
asasi za kiraia na kadhalika. Makundi zaidi ya 160 yalikutana na Tume na kutoa maoni.
Tume pia ilipata maoni ya viongozi wa juu wa Serikali walioko madarakani na waliostaafu.
Kwa jumla viongozi 43walitoa maoni.
Tume ilipanga kutumia miezi mitatu ya Februari,
Machi na Aprili kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba. Lakini tuligundua
kwamba maoni tuliyopata yalikuwa mengi sana, na pamoja na matumizi ya teknolojia ya
kisasa, tulitambua umuhimu wa kuongeza muda hadi mwisho wa mwezi Mei, Maoni ya wananchi
yaligusa mambo yote yanayohusu Katiba na mengi ya maoni hayo yalikinzana. Aidha, baadhi
ya maoni yaligusia masuala ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji. Tulifanya uchambuzi
makini na wa ndani wa maoni hayo na kazi hiyo tumeikamilisha na rasimu imeandaliwa
na Tume na leo tupo hapa kwa ajili ya kuizindua, ambapo Wananchi watapata nafasi ya
kuisoma. Kwa leo, kwa niaba ya Tume, napenda kutaja maeneo machache tu ambayo tunayapendekeza.
2.0.
IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA Ndugu Wananchi, Katiba yetu ya
sasa ina ibara 152. Tume ilifanya jitihada kubwa sana kuandaa rasimu ambayo siyo ndefu.
Lakini katika hali halisi haikuwezekana. Rasimu ya Katiba tunayopendekeza ina ibara
240.
3.0. MISINGI MIKUU YA TAIFA Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio unaobeba
misingi mikuu ya Taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Tume inaamini kwamba
misingi hii ni mizito na inastahili kubaki kwenye Katiba mpya. Hata hivyo, Tume imeona
ni busara kuongeza misingi mingine mitatu ya Usawa, Umoja na Mshikamano. Hivyo, Tume
imependekeza Katiba iwe na Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu,
Usawa, Umoja, Amani na Mshikamano.
4.0. TUNU ZA TAIFA Katiba yetu ya sasa
haina sehemu inayoelezea tunu za Taifa (National Values). Wananchi wengi walitoa maoni
kwamba Katiba itaje Tunu za Taifa. Tume imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani
ya Katiba. Tunu hizo ni;- Utu, 4. Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji
na Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.
5.0. MALENGO YA TAIFA Tume ilipozunguka
nchi nzima wananchi walizungumzia sana kuhusu malengo ya taifa. Walitaka Katiba ionyeshe
dira ya taifa. Wananchi wanayo ndoto yao ya Tanzania ya kesho na kesho kutwa. Kwa
kuzingatia maoni ya wananchi, kuna sura nzima inayohusu Malengo mahsusi na ya msingi
ya mwelekeo wa shughuli za Kiserikali na Sera za Kitaifa. Rasimu ya Katiba inaeleza
kuwa Malengo ya Kitaifa yaliyoainishwa ndani ya Rasimu yatakuwa ni Mwongozo kwa Serikali,
Bunge, Mahakama, Vyama vya Siasa, Taasisi na Mamlaka nyingine, na kwa kila mwananchi
katika matumizi au kutafsiri Masharti ya Katiba au Sheria nyingine za Nchi.
Kwa
msingi huo, Tume imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa mpangilio wa kuonesha
malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kimazingira na sera ya mambo ya
nje. Malengo hayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba.
6.0. VYOMBO VYA KIKATIBA Wananchi
walizungumzia suala la kubainishwa kwa vyombo vya Kikatiba na kuingizwa kwenye Katiba
ili viwe na nguvu ya Kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yao. Tume imependekeza
baadhi ya vyombo vifuatavyo viwe vya Kikatiba; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali,
Baraza la Mawaziri, Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri;
Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora
7.0. MAADILI YA VIONGOZI NA MIIKO YA UONGOZI Wananchi
wengi pia walizungumzia kwa upana sana kuhusu maadili na miiko ya Viongozi, kwa kuzingatia
maoni ya wananchi Tume inapendekeza maadili ya viongozi wa umma, pamoja na miiko ya
uongozi yawekwe kwenye Katiba. Tume pia imependekeza kuwa Sekretariati ya Maadili
ibadilishwe kuwa Tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja
miiko ya uongozi.
8.0. HAKI ZA BINADAMU Kuhusu haki za binadamu wananchi
walitaka haki hizi ziimarishwe na kusiwe na vikwazo visivyo vya lazima. Tume imependekeza
mabadiliko katika baadhi ya haki za binadamu kwa madhumuni ya kuziimarisha. Moja ya
mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru wa mwananchi kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza
kwamba vikwazo vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume
inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.
Tume pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe
kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, , haki ya mtoto, haki za Watu
wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Makundi Madogo katika Jamii,
Haki ya Elimu na Kujifunza, Haki ya kupata habari, Haki na uhuru wa habari na vyombo
vya habari na kadhalika.
9.0. URAIA Wananchi wengi walipendekeza kuwa suala
la Uraia libainishwe wazi kwenye Katiba. Tume imependekeza kwa kutaja Raia wa Jamhuri
ya Muungano na haki zake.
10.0. MIKOPO NA DENI LA TAIFA Ndugu Wananchi, Wananchi
walizungumzia suala la uwepo wa Ukomo wa nchi kukopa na uwepo wa utaratibu wa kulipa
Deni la Taifa ili kuilinda Nchi isiwe na deni kubwa. Kwa kuzingatia
maoni ya
Wananchi, Tume imependekeza kuwa, Serikali itawajibika kutoa taarifa Bungeni kuhusu
Mikopo kwa kuainisha kiasi cha deni lililopo, riba yake na matumizi ya fedha za Mikopo
na utaratibu wa kulipa Madeni ya Taifa.
11.0. MFUMO WA UTAWALA Kuhusu utawala,
Tume inapendekeza Tanzania iendelee na mfumo wa Jamhuri kwa maana ya nchi inayoongozwa
na Rais Mtendaji ambaye ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
12.0.
UCHAGUZI WA RAIS 12.1. Umri wa kugombea Urais Tume ilipokea maoni yanayokinzana
kuhusu umri wa mwananchi kugombea Urais. Baadhi walipendekeza mtu akishakuwa na sifa
ya kupiga kura awe pia na sifa ya kugombea Urais. Umri wa mtu kuruhusiwa kupiga kura
ni miaka 18. Wengine walipendekeza umri uliopo kwenye Katiba wa mtu kugombea Urais,
yaani kuanzia miaka 40 na kuendelea, uendelee kubaki kama ulivyo.
Wengine walisema
Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea Urais uwe miaka 35 au miaka 50 na kuendelea. Tume
imeyachambua maoni yote hayo, ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za Nchi zingine
na uhalisia wa watu wanaogombea na kuchaguliwa kuwa Marais katika Nchi mbalimbali
Duniani ambazo zingine zimeruhusu wagombea wa nafasi ya Urais kuwa na umri chini ya
miaka 40. Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi.
Kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na hali halisi, Tume inapendekeza Rais aendelea
kuchaguliwa na wananchi na pamoja na sifa nyingine, mtu anayeomba urais asiwe chini
ya miaka 40.
Uchaguzi wa Rais itakuwa kama ilivyo sasa, yaani mgombea Urais
atakuwa na mgombea mwenza kwa utaratibu kama ilivyo sasa. Isipokuwa, Tume imependekeza
Mgombea Urais anaweza kupendekezwa na Chama cha Siasa au kuwa Mgombea Huru. Mgombea
wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia
hamsini ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza
kulalamikiwa Mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi. Wanaoweza kufungua
kesi ni wagombea Urais. Aidha, ni Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na Mamlaka na
uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima
liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku therathini. Rais aliyeshinda ataapishwa
siku thelathini tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na Mahakama.
13.0.
MADARAKA YA RAIS Ndugu Wananchi, Tume inapendekeza kwamba, Rais abaki na madaraka
ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Hata hivyo inapendekezwa Rais ashirikiane na
taasisi na vyombo vingine katika uteuzi. Kwa mfano: Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu
Waziri, Rais atateua na Bunge litathibitisha. Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu
Rais atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya Uutumishi wa
Mahakama na baada ya hapo Bunge litathibitisha. Kuhusu Wakuu wa vyombo vya Ulinzi
na Usalama inapendekezwa kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Ulinzi na
Usalama la Taifa, ambalo kati ya majukumu yake itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi
wa Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Kuhusu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma.
14.0.
KINGA YA RAIS Tume baada ya kupitia maoni ya Wananchi, inapendekeza Rais abaki
na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushitakiwa na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.
15.0.
IDADI YA MAWAZIRI Inapendekezwa Rais aunde Serikali ndogo iliyo na Mawaziri wasiozidi
kumi na tano na mawaziri hao wasiwe wabunge. Mawaziri hawatahudhuria vikao vya Bunge
isipokuwa kama watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.
16.0. BUNGE Ndugu
Wananchi, Kuhusu Bunge kutakuwa na wabunge wa aina mbili. Kutakuwa na Wabunge wa
kuchaguliwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha Watu wenye Ulemavu. Kila
Jimbo la Uchaguzi litakuwa na Wabunge Wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Tume
inapendekeza kwamba, Mbunge akifukuzwa na Chama cha Siasa abaki kuwa Mbunge lakini
akihama Chama atapoteza Ubunge wake. Inapendekezwa ukomo wa Ubunge uwe vipindi
vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao
kabla ya mwisho wa kipindi chake. Inapendekezwa pia kusiwepo na uchaguzi mdogo
isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na Mbunge huru ndipo utafanyika uchaguzi
mdogo kujaza nafasi hiyo, lakini kama nafasi ikiwa wazi kutokana na Mbunge wa Chama
cha Siasa basi nafasi hiyo, ijazwe na mtu kutoka Chama hicho. Inapendekezwa Spika
na Naibu Spika wasitokane na Wabunge na wasiwe Viongozi wa vyama vya Siasa.
17.0.
TUME YA UCHAGUZI Tume imefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi kuhusu Tume ya Uchaguzi.
Tume inapendekeza jina la tume liwe Tume Huru ya Uchaguzi. Tume pia inapendekeza sifa
za wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ziwekwe kwenye Katiba. Wajumbe wa Tume Huru ya
Uchaguzi watapatikana kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya
Katiba kwa kuomba. Majina ya waombaji yatachambuliwa na Kamati ya Uteuzi ambayo Mwenyekiti
wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni Majaji Wakuu wa nchi Washirika,
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Maspika wa Mabunge wa nchi Washirika na Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu.
Kamati ya uteuzi itapendekeza majina ya watu wanaofaa
kwa Rais ambaye atateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine. Bunge litathibitisha
uteuzi wao. Wabunge na viongozi wa aina hiyo hawatakuwa na sifa za kuwa wajumbe wa
tume ya uchaguzi. Inapendekezwa Tume huru ya Uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi,
kura ya maoni na Usajili wa Vyama vya Siasa.
18.0. MAHAKAMA Kuhusu Mahakama
inapendekezwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) Majaji wa Mahakama ya
Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi
wa Mahakama.
19.0. MUUNDO WA MUUNGANO Ndugu Wananchi, Suala la muundo
wa Muungano ndilo lililokuwa gumu kuliko masuala yote. Tume ilitumia muda mwingi kuchambua
maoni ya wananchi. Pamoja na kwamba hadidu za rejea zilielekeza Tume kuzingatia uwepo
wa Muungano, baadhi ya wananchi walitoa maoni kwamba Muungano uvunjwe na Tume iliyapokea
maoni hayo. Licha ya kwamba waliotaka kuvunjwa muungano walikuwa wachache sana, Tume
ilichambua sababu walizotoa na kuridhika kwamba hazikuwa na uzito.
Wananchi
walio wengi walitaka Muungano uendelee. Kati yao wapo waliopendekeza Muungano wa Serikali
moja, Serikali mbili, Serikali tatu, Serikali nne na muungano wa mkataba. Sababu za
wale waliopendekeza Serikali nne hazikuwa na uzito, kwa hiyo Tume ikaamua kutopendekeza
muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Serikali moja walikuwa wachache lakini
sababu zao zilkuwa na uzito. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia hali halisi iliona ni
changamoto kubwa kuwa na Muungano wa Serikali Moja
Wananchi waliopendekeza
Muungano wa Mkataba walikuwa wengi (hasa wananchi wa Zanzibar) na sababu zao zilikuwa
na uzito. Lakini uchambuzi wa Tume ilionekana wazi kwamba ili kupata mkataba lazima
kwanza kuwe na nchi mbili huru kabisa lakini hakukuwa na mazingira ya uhakika ya kupata
mkataba wa muungano. Tume iliona kuna changamoto ya muungano kuvunjika ingawa waliotoa
maoni walisisitiza muungano ubaki. Hivyo, Tume iliamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi
waliopendekeza Tanzania iendelee na Muundo wa sasa wa Serikali mbili walikuwa wengi
na sababu zao zilikuwa nzito. Hata hivyo, wananchi katika kundi hili walipendekeza
mabadiliko mengi na makubwa. Tathmini ya Tume ilionyesha kwamba isingewezekana kufanya
mabadiliko yote yaliyopendekezwa.
Wananchi waliopendekeza muundo wa Serikali
tatu walikuwa wengi kuliko makundi yote. Sababu zao zilikuwa nzito lakini pia kulikuwa
na changamoto nyingi na nzito. Pamoja na maoni ya wananchi Tume ilirejea sababu za
kupendekeza muundo huu zilizotolewa na Tume zilizopita na Tafiti zilizofanywa na Tume
kuhusu aina mbalimbali za Muungano. Baada ya yote hayo Tume ilifikia uamuzi wa kupendekeza
mfumo wa Serikali tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
20.0. ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO Ndugu
Wananchi, Tume imependekeza katika Rasimu ya Katiba kuwa orodha ya Mambo ya Muungano
yawe 7 badala ya 22 yaliyopo sasa. Mambo ya muungano yanayopendekwa ni: 1. Katiba
na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2. Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania 3. Uraia na Uhamiaji 4. Sarafu na Benki Kuu 5. Mambo
ya Nje 6. Usajili wa Vyama vya Siasa 7. Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya
Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
21.0. BENKI KUU Kwa kuwa Tume imependekeza
Muungano wa Shirikisho kutokana na uzito wa maoni ya wananchi. Hivyokutakuwa na Benki
Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusimamia masuala
ya Sarafu na Fedha za Kigeni na Benki za Washirika wa Muungano.
22.0. BENKI
ZA SERIKALI ZA WASHIRIKA Kutokana na pendekezo la kuwepo kwa Serikali ya Shirikisho
la Nchi tatu, inapendekezwa kuwepo kwa Benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti
ya fedha za Serikali za kila Mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki za biashara
katika mamlaka zao.
23.0. BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU YA KATIBA 23.1.
Serikali ya Majimbo Ndugu Wananchi, Tume ilipokea maoni kuhusu mambo mengine
muhimu ambayo hayamo katika rasimu hii. Moja ya mambo hayo ni Serikali za Majimbo.
Tume ilichambua maoni na sababu za wananchi kupendekeza Serikali za Majimbo lakini
Tume ilibaini changamoto nyingi na ikaamua kutopendekeza muundo huu. Kwanza, baada
ya kuamua kupendekeza Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, ilionekana ni dhahiri kuongeza
ngazi nyingine ya Serikali ingeleta gharama kubwa. Serikali nyingine kumi zingekuwa
na Wakuu wa Majimbo, Mabaraza ya Mawaziri na Mabunge na gharama yake ingekuwa kubwa.
Pili,
katika kutembelea nchi Tume ilishuhudia dalili za wazi za mivutano ya Udini, ukanda,
malalamiko ya upendeleo wa baadhi ya maeneo na ukabila. Dalili zilikuwa wazi kwamba
utawala wa majimbo ungeirudisha nchi kwenye utawala utakaoigawa nchi kwa misingi ya
ukabila, udini na ukanda na kuzigawa rasilimali za taifa kikanda na hivyo kuleta tofauti
kubwa ya kimaendeleo katika nchi.
23.2. Mahakama ya Kadhi Ndugu wananchi, Jambo
la pili ni mahakama ya kadhi. Tume ilipokea maoni mengi kuhusu suala hili. Baadhi
ya wananchi walitaka mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba na wengine walipinga.
Baada ya kuamua kuwa Muundo wa Muungano uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona kuwa Mahakama
ya Kadhi siyo suala la Muungano na imeliacha ili lishughulikiwe na Washirika wa Muungano. Hata
hivyo ilionekana kuwa suala siyo kuwapo au kutokuwapo kwa mahakama ya kadhi. Mahakama
hizo zinaweza kuwapo bila ya kuwa katika Katiba. Zanzibar kuna mahakama ya kadhi bila
kuingizwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Kwa kutumia uzoefu huo hata Tanzania Bara inaweza
kupata ufumbuzi wa suala hili.
23.3. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya Jambo
la Tatu ni Kuwepo au kutokuwepo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Baadhi ya Wananchi walitaka
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasiwepo, wengine walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee
kuwepo lakini wachaguliwe na wananchi na waengine wakasema wawepo na waendelee kuteuliwa
na Rais kama ilivyo sasa. Tume ilitafakari kuhusu suala hili na kuamua kwamba siyo
suala la Muungano na kwa kuwa Muundo wa Muungano imependekezwa uwe wa Serikali Tatu,
Tume iliona suala la uwepo au kutokuwepo na namna ya upatikanaji wa Wakuu wa Mikoa
na Wilaya lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
23.4. Serikali za Mitaa Kuhusu
Serikali za Mitaa, Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi kuhusu kuziimarisha Mamlaka
za Serikali za Mitaa kwa kuzipatia uhuru kamili wa kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa
na Serikali Kuu. Tume ilitafakari suala hili na kuamua kwamba siyo jambo la Muungano
na hivyo, litashughulikiwa kwenye Katiba za Washirika wa Muungano.
23.5. Uraia
wa Nchi mbili Ndugu Wananchi,
Jambo la tatu ni Uraia wa Nchi mbili. Tume
ilipokea maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kuwekwa kwenye Katiba suala la
Uraia wa nchi mbili. Baada ya kufanya uchambuzi kwa kutengenisha mambo yapi ni ya
Kikatiba na yapi yanaweza kutekelezwa bila kuingizwa kwenye Katiba bali kwenye Sheria
inayohusu jambo husika, Tume imependekeza kuwa suala la Uraia wa nchi mbili linaweza
kuwekwa kwenye Sheria badala ya kuwekwa kwenye Katiba. hii ni kwa sababu kutokana
na utafiti uliofanywa na Tume, suala hilo linaweza kubadilika wakati wowote na hivyo
likiwa kwenye Katiba linaweza kuifanya Katiba kubadilishwa mara kwa mara.
24.0.
MWISHO Naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Tume kuwashukuru Watanzania wote
kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, kuanzia hatua ya
kutoa maoni na kuwachagua wawakilishi wenu watakaopata fursa ya kuipitia, kuijadili
na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba. Ushirikiano huu ulikuwa muhimu sana kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba hasa ukizingatia kuwa lengo ni kupata Katiba Mpya ambayo itaakisi
ndoto na matakwa ya Wananchi wa Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inatoa
shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar: 1. Kwa kuipatia vifaa afisi na mahitaji ya lazima 2. Kwa kuiwezesha
Tume kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, 3. Kwa kutokuingilia Uhuru wa Tume
wakati wa Utekelezaji wa Majukumu yake na 4. Kutoa Wataalam wenye Weledi, Mahiri,
Makini na Waadilifu ambao wameunda Sekretarieti ya Tume.
Ndugu Wananchi, Shukrani
za pekee ziwaendee: 1. Wakuu wa Mikoa, 2. Wakuu wa Wilaya, 3. Wakurugenzi
/ Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, 4. Makamanda wa Polisi wa Mikoa na
Wilaya, 5. Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na Masheha. Kwa kuisaidia Tume kutekeleza
Majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, tunazishukuru Asasi za Kiraia, Taasisi, Jumuiya
za Kidini, Vyama vya Siasa na Makundi mbalimbali kwa namna walivyoshiriki katika kuhamasisha
wananchi kushiriki katika kutoa maoni. Mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, Tunawashukuru
Wanahabari wote kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuisaidia Tume kufikisha taarifa mbalimbali
za Tume kwa Wananchi na katika kuhamasisha Wananchi kushiriki katika mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba. Nachukua nafasi hii kuwaomba Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya, Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo yanyofanana
kushiriki vyema, kwa umakini, utulivu na kwa amani katika hatua hii ya kuipitia, kuijadili
na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba. Tume imekuwa ikithamini na itandelea kuthamini
mawazo na maoni kutoka kwa Watanzania wote. Rasimu ya Katiba itapatikana kwenye
tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya www.katiba.go.tz SASA NAKUOMBA MHESHIMIWA
MAKAMU WA RAIS UIZINDUE RASMI RASIMU YA KATIBA Ahsanteni kwa kunisikiliza. TOA
MAONI TUPATE KATIBA MPYA